Baada ya kutimuliwa Russia, shirika la uhajiri wa Mayahudi kuhamishiwa Israel

Sambamba na kushadidi mivutano katika uhusiano wa Russia na Israel, duru za habari zimeripoti kuwa shirika la uhajiri wa Mayahudi limeandaa mpango wa siri wa kuhamishia Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) ofisi yake iliyokuweko mjini Moscow.

Gazeti la Jerusalem Post limezinukuu duru za kuaminika zikiripoti kuwa kufuatia uamuzi wa Russia wa kuifunga ofisi ya shirika la uhajiri wa Mayahudi mjini Moscow, hatua ambayo imewakasirisha sana viongozi wa utawala wa Kizayuni, shirika hilo limeandaa mpango wa siri wa kuhamishia ofisi yake Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuendesha operesheni na shughuli za uhamishaji wa Wayahudi kutokea nje ya ardhi hizo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, uamuzi huo umechukuliwa baada ya wizara ya sheria ya Russia kutoa amri ya kusimamishwa shughuli za shirika hilo katika ardhi ya nchi hiyo kwa kile kilichotajwa kuwa ni “ukiukaji wa sheria za Russia”.

Kutokana na hatua hiyo iliyochukuliwa na Russia, utawala wa Kizayuni wa Israel unajipanga kuchukua hatua kadhaa za kulipiza kisasi dhidi ya Moscow.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *