Balozi mpya wa Iran nchini Iraq, Mohammad Kazem al-Sadegh, amewapongeza wabunge wa Bunge la Iraq kwa kuipigia kura sheria inayoharamisha uhusiano na utawala ghasibu wa Kizayuni.
Al-Sadegh aliandika katika ukurasa wake wa kibinafsi wa Twitter: “Tunawapongeza wawakilishi wa taifa ndugu la Iraq katika bunge kwa kuipigia kura sheria ya kihistoria inayoharamisha uhusiano na utawala huo ghasibu wa Kizayuni, ambayo ni hatua mpya ya kujivunia katika mfululizo wa misimamo ya fahari na kijasiri ya wananchi wa Iraq katika masuala muhimu ya Umma wa Kiislamu..”
Bunge la Iraq lilipiga kura siku ya Alkhamisi kuhusu muswada unaoharamisha uhusiano na utawala wa Kizayuni.
Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Bunge ilitoa taarifa na kutangaza: Katika kikao cha leo cha kupitia sheria inayopendekezwa, kura ya kauli moja ilipigwa mbele ya wawakilishi waliohudhuria.
Madhumuni ya sheria hii ni kuharamisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kwa njia yoyote ile na kuzuia uanzilishaji wa uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na utawala huo.