Balozi wa Kenya nchini Iran atembelea viwanda vya uzalishaji Arak

Balozi wa Kenya mjini Tehran ametembelea viwanda vya uzalishaji katika mji wa Arak, makao makuu ya mkoa wa Markazi, unaofahamika kama mji mkuu wa viwanda wa Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Joshua Gatimu, Balozi wa Kenya nchini Iran alizitembelea kampuni hizo za uzalishaji yakiwemo mashirika ya kuzalisha dawa jijini Arak jana Jumapili.

Katika mahojiano na Iran Press pambizoni mwa ziara yake hiyo mjini Arak katikati ya Iran, Balozi Gatimu ameashiria safari ya hivi karibuni Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Kenya na kusema kuwa, anatumai ziara hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa nchi mbili.

Amesema, “Kwa bahati nzuri, safari ya Rais wa Iran nchini Kenya ilikuwa na mafanikio, na natumai yatakuwa na matokeo chanya. Nipo tayari kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa na nchi mbili hizi katika safari hiyo.”

Mwanadiplomasia huyo wa Kenya amebainisha kuwa, wajumbe wa Kenya karibuni hivi wataitembelea Iran kuzungumza na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, na kufuatilia utekelezaji wa mapatano yaliyosainiwa katika safari ya Rais Raisi mjini Nairobi.

Balozi wa Kenya mjini Tehran jana alitembelea shirika la ‘Combine Sazi’ la kuzalisha mashine za kilimo lililoasisiwa 1969 mjini Arak na ‘Behrood Atrak’ ya kuzalisha madawa.

Aidha ameitembelea kampuni ya ‘Avangplast’ ya kuzalisha mapipa, na pia inatambulika kama mzalishaji mkubwa zaidi wa nguzo na vigingi vya kusambaza umeme katika eneo la Asia Magharibi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *