Balozi wa Palestina aitaka jumuiya ya kimataifa kuilaani Israel

Haya ni maneno ya Balozi wa Palestina nchini Tanzania akiitaka Jumuiya ya kimataifa ilaani vitendo vya utawala haramu wa Israel kama inavyolaani vitendo vya Russia huko Ukraine,

Dar es Salaam. Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Hamdi Mansour Abuali ameitaka jumuiya ya kimataifa kulaani vitendo vya Israel kukiuka makubaliano na Palestina kama ambavyo wamekuwa wakilaani uvamizi wa Russia huko Ukraine.

Abuali ametoa wito huo leo Alhamisi Aprili 21, 2022 wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mataifa mbalimbali yanavyojitokeza kulaani uvamizi wa Russia nchni Ukraine lakini hakuna anayelaani unyanyasaji wa Waisrael kwa Wapalestina.

Amesema zaidi ya nyumba 2000 za Wapalestina zimebomolewa katika mji wa Jerulasem kwa sababu Waisrael hawataki Wapalestina wawe na makazi katika mji huo badala yake wanataka wawe Wayahudi pekee.

“Tulikuwa na makubaliano, tunataka utekelezaji wa hayo makubaliano, kuwa na taifa la Palestina. Lakini sasa Israel imebadilisha mawazo, hawatii hayo makubaliano, hakuna anayelaani hilo,” amesema Balozi Abuali.

Amesema kama kungekuwa na msukumo kwa Israel kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na Palestina, kungekuwa na nafasi ya kuwa na taifa la Palestina, lakini inashindikana kwa sababu hawapati msukumo huo.

Israel ilitekeleza mauaji ya watu 1400 huko Gaza lakini hakuna aliyelaani kitendo hicho na Israel inajua kwamba haipati msukumo huo

“Ni matamko mangapi yametolewa kulaani vitendo vya Waisrael? Kwa hiyo, wamejenga dhana ya kufanya chochote kwa sababu hakuna mtu wa kuwakemea. Njia pekee ya kuilazimisha nchi kufuata utaratibu ni kuiwekea vikwazo, lakini hatuoni kwa Israel,” amesema Balozi huyo.

Balozi Abuali amesema mwaka 1973, Mwalimu Julius Nyerere alionyesha mfano wa kuweka msukumo kwa Ubalozi wa Israel nchini Tanzania kwamba wasipofuata azimio la Umoja wa Mataifa (UN) hatakubaliana nao.

Moja ya makubaliano yaliyofikiwa wakati huo ni kwamba Waisrael wataachia maeneo yanayokaliwa na Wapalestina na walipeana muda wa kutekeleza makubaliano hayo lakini Waisrael hawataki kufuata makubaliano hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *