Ubalozi wa Russia nchini Iran umejibu ujumbe wa Twitter wa balozi wa Uingereza nchini Iran kuhusu matukio ya Ukraine na kusema, madola ya Magharibi hayana ustahiki wa kuilaani Russia.
Balozi wa Uingereza nchini Iran Simon Schercliff, amesambaza picha katika ukurasa wake wa Twitter inayoonesha bendera ya Ukraine ikiwa imepandishwa katika Ubalozi wa Uingereza mjini Tehran. Picha hiyo iliandamana na maandishi yasemayo: “Tumepandisha bendera ya Ukraine kama njia ya mshikamano na marafiki wetu Ukraine.”
Katika kujibu ujumbe huo, Ubalozi wa Russia nchini Iran umekosoa matamshi hayo ya Simon Schercliff huku ukizikejeli nchi za Magharibi ambazo zimekuwa zikiingilia kijeshi na kueneza vita kote duniani.
Ujumbe wa Ubalozi wa Russia umesema: “Kwa kuzingatia ukosoaji wa nchi za Magharibi kuhusu oparesheni maalumu za kijeshi za Russia nchini Ukraine, hasa ujumbe wa twitter wa Simon Shercliff, Ubalozi wa Russia unasema hivi: Wale ambao walidondosha mabaomu katika mijil iliyokuwa na amani ya Serbia mwaka 1999, wale ambao walivamia Iraq kijeshi kinyume cha sheria mwaka 2003, kisha wakaziharibu Libya na Syria na kutoroka kwa madhila Afghanistan hawana ustahiki wa kimaadili wa kuilaani Russia.”
Rais Vladimir Putin wa Russia mapema Alhamisi alihutubia taifa katika televisheni na kutangaza kuwa, vikosi vya nchi yake vimeanza oparesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass ambalo limetangaza kujitenga na Ukraine. Punde baada ya kutangaza oparesheni hiyo ya kijeshi, Putin ametaka kusitishwe ‘muundo wa kijeshi’ Ukraine na kuitaka nchi hiyo iweke chini silaha zake.
Kama ilivyotarajiwa, baada ya Russia kutambua uhuru wa maeneo mawili ya Donetsk na Lugansk, yaliyotangaza kujitenga na Ukraine, maeneo hayo yalimuomba msaada Rais Putin na kwa msingi huo mapema Alhamisi 24 Februari Russia ilianzisha oparesheni kubwa za kijeshi nchini Ukraine kwa kudondosha mabaomu katika vituo vya kijeshi na maghala ya silaha nchini humo.