Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York limepitisha kwa wingi mkubwa wa kura azimio la kuunga mkono haki ya kujitawala ya wananchi wa Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anatolia, Riyadh al-Maliki ameeleza kwamba azimio hilo limepitishwa katika kikao cha kawaida cha baraza kuu kwa wingi mkubwa wa kura za ‘ndiyo’ za nchi 168.
Al-Maliki ameongeza kuwa, wakati nchi sita za Chad, Israel, Visiwa vya Marshall, Micronesia, Nauru na Marekani zilipinga azimio hilo nchi zingine tisa ziliamua kutopiga kura.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekaribisha azimio hilo na kuzishukuru nchi zilizopiga kura za kuunga mkono.
Al-Maliki amesisitiza kwa kusema: “kura hizi zilizounga mkono ni jibu madhubuti na la kutarajiwa wale wanaojaribu kutilia shaka haki ya wananchi wa Palestina ya kujitawala na kujiamulia mustakabali wao kupinga na zinapinga pia hadharani ukiukaji wa haki za taifa letu unaofanywa na Israel na jinai za utawala huo”.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aidha amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza ahadi na wajibu wao wa kulinda haki za wazi za wananchi wa Palestina na kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha jinai za utawala unaokalia Quds tukufu kwa mabavu.
Mapema mwezi huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura maazimio matano ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hususan kuhusiana na suala la wakimbizi wa Kipalestina.