Baraza la Seneti Kenya lamuondoa madarakani Naibu Rais Gachagua

Baraza la Seneti nchini Kenya limeidhinisha uamuzi wa kumuondoa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua.

Jana Baraza la Seneti la Kenya lilipiga kura na kuidhinisha kuondolewa ofisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kutokana na mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Maseneta 54 kati ya 67 walipiga kura ya kumfukuza Gachagua kwa shtaka la kwanza la “ukiukaji mkubwa wa katiba”, zaidi ya theluthi mbili ya idadi inayohitajika kisheria, na kumfanya kuwa naibu rais wa kwanza kulazimishwa kuondoka madarakani kwa mashtaka kama hayo.

Gachagua, ambaye amekanusha madai hayo, alipaswa kujitetea dhidi ya mashtaka katika Seneti Alhamisi alasiri kabla ya upigaji kura. Alipokosa kufika, wakili wake Paul Muite alisema naibu huyo wa rais alikuwa amelazwa hospitalini akiwa na maumivu makali ya kifua, na kuitaka Seneti kusitisha shughuli kwa siku kadhaa.

Lakini seneti ilikataa kufanya hivyo, na kupelekea timu ya wanasheria wa Gachagua kupinga hatua hiyo na kuondoka bungeni.

Gachagua anakabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo za ufisadi, kukiuka katiba, kumhujumu rais na kushajiisha migawanyiko ya kikabila. Gachagua anakuwa Naibu Rais wa kwanza kuvuliwa mamlaka na Bunge chini ya Katiba ya 2010.

Itakumbukwa kuwa, Bunge la Kitaifa la Kenya siku ya Jumanne lilipasisha kwa wingi wa kura hoja ya kumng’oa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.

Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 yaliyojumuisha ulimbikizaji wa mali ya Shilingi bilioni 5.2 za Kenya kupitia njia za ufisadi katika miaka miwili akiwa naibu rais pamoja na madai ya kuwagawanya Wakenya kwa kauli yake kwamba serikali ya Kenya Kwanza imeundwa na ‘wenye hisa’ pekee.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *