Baraza la Usalama lakataa kuchunguza maabara za kibiolojia za US Ukraine

Nchi za Magharibi kwa mara nyingine tena zimelitumia vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kuzuia ombi la Russia la kutaka kufanyika uchunguzi kuhusu uwepo wa maabara za silaha za kibiolojia za Marekani nchini Ukraine.

Marekani, Ufaransa na Uingereza zimelipigia veto ombi hilo la Russia, ambalo hata hivyo limeungwa mkono na China. Nchi 10 wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimejizuia kulipigia kura pendekezo hilo la Russia.

Dmitry Polyansky, Naibu Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, amesikitishwa mno na hatua hiyo ya Marekani, Ufaransa na Uingereza ya kutumia turufu kukwamisha ombi hilo muhimu la Moscow.

Nchi hizo za Magharibi zinadai kuwa, pendekezo hilo la Russia limetokana na taarifa zisizo sahihi, na linaonesha ukosefu wa uaminifu na nia njema ya Moscow, mbali na kuikosoa heshima taasisi hiyo.

Russia hivi karibuni ilipeleka malalamiko yake rasmi kwa Umoja wa Mataifa kuhusu kuwepo kwa maabara za silaha za kibiolojia za Marekani nchini Ukraine.

Vasily Nebenzia, ​​mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amethibitisha kwamba nchi yake imekusanya ushahidi wa kutosha kuhusu uwepo wa maabara hizo za silaha za kibiolojia za Marekani huko Ukraine.

Aidha hivi karibuni, Rais Vladimir Putin wa Russia alionya kuhusu nchi za Magharibi kuitumia Ukraine kama uwanja wa majaribio ya silaha zao za kibiolojia na kemikali.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *