Bei za bidhaa UK zavunja rekodi ya miaka 20; vita Ukraine moja ya sababu

Utafiti wa karibuni kabisa unaonesha kuwa, bei za bidhaa muhimu zimepaa vibaya nchni Uingereza na kuvunja rekodi ya miongo miwili iliyopita, suala ambalo limepandisha mno ughali wa maisha. Wataalamu wa mambo wanasema, vita vya Ukraine na kitendo cha nchi za Magharibi cha kuiwekea vikwazo Russia kimechangia sana katika hali hiyo mbaya ya maisha huko Uingereza.

Shirika la habari la IRNA limenukuu matokeo ya utafiti huo mpya kabisa uliofanywa na mashrika ya BRC na Nielsen yakionesha kuwa, mfumuko wa bei za bidhaa muhimu nchini Uingereza ulifikia asilimia 13.3 mwezi uliopita wa Disemba, 2022 na huo ni uthibitisho wa kuendelea kupanda ughali wa bidhaa ikilinganishwa na miezi ya kabla yake.

Mfumuko wa bidhaa muhimu na kupanda gharama za maisha nchini Uingereza kumewatumbukiza wananchi wa nchi hiyo ya Ulaya katika wakati mgumu sana kiasi kwamba uchunguzi mwingine wa maoni unasema, asilimia kubwa ya raia wa Uingereza wanaamini serikali yao ilifanya makosa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Matokeo ya uchunguzi huo mpya yanaonesha kuwa, mfumuko wa bei na kupanda gharama za maisha nchini Uingereza kumeongezeka kutoka takriban asilimia 2 na kufikia asilimia 10.7 katika miezi ya hivi karibuni huku mchakato huo ukiendelea kuwa mkubwa na maisha yakizidi kuwa magumu katika mkoloni huyo kizee wa barani Ulaya.

Uchunguzi huo unaonesha pia kuwa, bei za bidhaa muhimu zitaendelea kupaa nchini Uingereza katika mwaka huu mpya wa 2023.

Ugumu wa maisha ni mkubwa sana nchini Uingereza kiasi kwamba mamia ya maelfu ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali, kuanzia za reli hadi za wauguzi na madereva wa magari ya wagonjwa wameshiriki katika mgomo mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *