Waendesha mashtaka wa Benin wametangaza kuwa watu watatu mashuhuri, akiwemo kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais, wamekamatwa kwa tuhuma za kupanga njama ya “mapinduzi” katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi.
Washukiwa wengine wawili katika tuhuma za jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Benin ni waziri wa zamani wa michezo na mfanyabiashara anayetajwa kuwa karibu na Rais Patrice Talon wa nchi hiyo.
Elonm Mario Metonou, Mwendesha Mashtaka Maalumu katika Mahakama ya Benin kwa ajili ya uhalifu wa kifedha na ugaidi, amefichua kwamba mapinduzi hayo yalipangwa kutekelezwa siku ya leo Ijumaa.
“Inaonekana kamanda wa Republican Guard anayesimamia usalama wa rais alishirikiana na waziri Oswald Homeky na Olivier Boko ili kutekeleza mapinduzi kwa nguvu leo Septemba 27, 2024,” amesema Mwendesha Mashtaka wa Benin.
Kwa mujibu wa taarifa ya mahakama ya Benin, kamanda Homeky alizuiliwa mwendo wa saa saba usiku ya Jumanne wakati akikabidhi mifuko sita ya fedha, jumla ya faranga za CFA bilioni 1.5 za Afrika Magharibi (sawa na karibu dola milioni 2.5), kwa kamanda, Djimon Dieudonne Tevoedjre.
Boko, rafiki wa muda mrefu wa Rais Talon, alikamatwa usiku wa kuamkia Jumanne huko Cotonou, mji mkuu wa kiuchumi wa Benin. Alikuwa amedokeza hivi majuzi juu ya uwezekano wa kugombea urais mwaka 2026, baada ya kumalizika kwa muhula wa pili wa Talon.