Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kujiri maafa makubwa katika jimbo la California nchini humo kufuatia kimbunga mafuriko makubwa katika maeneo ambayo tayari yamejaa maji na wakati huo huo kuwepo uwezekano wa kunyesha theluji kufikia hadi mita mbili sawa na (futi sita).
Jumamosi jioni Rais wa Marekani alitangaza kuwa maafa makubwa yamelikumba jimbo la California na kuagiza serikali kutoa msaada kwa nchi hiyo sambamba na kufanyika juhudi za uokoaji katika maeneo yaliyoathirika na kimbunga cha msimu wa baridi kali, mafuriko, maporomoko ya udongo katika jimbo hilo.
Taarifa ya White House imeeleza kuwa, misaada kwa waathirika wa mafuriko huko California ni pamoja na kuwapatia makazi ya muda na kukarabatiwa nyumba zao, kupatiwa mikopo nafuu ili kudhamini mahitaji yao pamoja na mipango mingine ili kuwasaida wananchi na wamiliki wa biashara kujikwamua na taathira za maafa hayo.
Hadi sasa watu wasiopungua 19 wamefariki dunia kwa kimbunga hicho jimboni California. Miongoni mwa waliopoteza maisha huko California ni madereva waliopatikana katika magari yaliyozama chini ya maji, watu walioangukiwa na miti, pamoja na mume na mke waliokutwa wamefariki dunia chini ya mwamba. Aidha kuongezeka kina cha maji ya mvua na hali mbaya ya mambo zimesababisha kusitishwa kwa zoezi la kumtafuta mtoto wa kiume aitwaye Kyle Doan ambaye alisombwa na maji ya mafuriko wakati mama yake akijaribu kumvuta eneo salama kutoka ndani ya gari yao.