Shirika la Haki za Binadamu la Sanad limesema kuwa, viongozi wa Saudi Arabia wamewatia mbaroni makumi ya wanaharakati wa kike wanaopigania haki za wanawake nchini humo sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake.
Utawala wa kiimla wa Saudia unaendelea kukanyaga vibaya haki za wanawake. Kwa mujibu wa ripoti ya karibuni kabisa ya Shirika la Haki za Binadamu la Sanad, utawala wa kidikteta wa Aal Saud umewatia mbaroni wanaharakati 60 wa kisiasa katika miezi ya hivi karibuni na kufanya idadi ya wanawaharakati wa kike wanaopigania haki za wanawake na ambao wametiwa mbaroni nchini humo kufikia 100.
Televisheni ya al Alam imelinukuu shirika hilo likiongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sehemu kubwa ya wafungwa wa kike wa masuala ya itikadi wanateswa kiroho na kimwili katika seli za mtu mmoja mmoja.
Asma Al-Sabiei na Dk. Lina al-Sharif, Yasmin al-Ghafili, Aidah al-Ghamdi, Rina Abdulaziz n.k, ni miongoni mwa wanaharakati wakubwa zaidi waliotiwa mbaroni na viongozi wa Saudi Arabia.
Shirika la Haki za Binadamu la Sanad limesema kuwa, katika maadhimisho hayo ya kimataifa ambayo yanaadhimishwa katika kona mbalimbali duniani kila mwaka, yanapigania haki za wafungwa wanaoshikiliwa katika jela kutokana na itikadi zao, na kuushinikiza utawala wa kiimla wa Bin Salman ukomeshe dhulma zake huko Saudi Arabia.