Kadiri siku zinavyosonga mbele ndivyo faili la jinai za kivita la Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia na Sheikh Muhammad bin Zayed Al-Nahyan Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) huko nchini Yemen linavyozidi kuwa kubwa.
Licha ya vyombo vingi vya habari vya Magharibi kuelekeza macho na masikio yao katika vita vya Ukraine, lakini hii leo haiwezekani kupata sehemu yoyote ile duniani ambayo inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kama Yemen hususan watoto wa nchi hiyo.
Takwimu za hivi karibuni kabisa za Wizara ya Afya ya Yemen zinaonesha kuwa, watoto zaidi ya 80 wanaozaliwa nchini Yemen huaga dunia. Takwimu hizo zinaeleza kwamba, nchini Yemen watoto 1,120,000 huzaliwa kwa mwaka ambapo 39% kati yao ni watoto ambao huzaliwa kabla ya wakati. Hatua ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ya kutumia silaha zilizopigwa marufuku katika katika mashambulio yao huko Yemen kumepelekea kuongezeka idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao katika nchi hiyo. Katika hali ambayo, sekta ya afya na matibabu katika nchi hiyo inahitajia vifaa zaidi ya 2,000 vya kutunzi watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa sasa kuna vifaa 632 tu katika vituo vya afya. Hali hiyo inatajwa kuwa sababu kuu ya kuaga dunia watoto wengi wanaozaliwa kabla ya wakati kutokana na kukosekana vifaa hivyo.
Hisham Sharaf Abdullah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa amesema katika mazungumzo yake mjini Sana’a na Peter James Hawken, mwakilishi mkaazi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwamba, Yemen inakabaliwa na hali mbaya zaidi ya maafa ya kibinadamuu. Wanawake na watoto wa Yemen ndio tabaka lililoathiriwa zaidi na uvamizi, hujuma na mzingiro wa Saudii Arabia na waashirika wake.
Si hayo tu, bali hospitali nyingi nchini Yemen ima zimepata madhara makubwa au zimebomolewa kabisa. Hata hospitali zilizosalimika ni chache mno miongoni mwazo ambazo zinatoa huduma. Katika upande wa sekta ya elimu pia hali ni mbaya kwani akhari ya shule zimefungwa kutokana na vita na katika kila watoto watatu wa Kiyemen ni mtoto mmoja tu ndiye anaweza kwenda shule.
Licha ya kuwa watoto ndio tabaka lililo katika hatari zaidi katika vita hivyo vya Saudi Arabia na Imarati dhidi ya Yemen ikilinganiishwa na matabaka mengine katika jamii, lakini maafa hayo hayaishii kwa watoto tu, bali ni juimishi kwa watu wote. Zaidi ya 80% ya wananchi wa Yemen hivi sasa wanakabiliwa na maafa ya kibinadamu kutokana na vita, hujuma, mashambulio na mzingiro unaotekelezwa dhidi yao na mataifa mawili ya Kiarabu ya Saudia na Imarati pamoja na washirika wao.
Jumuiya na asasi za kimataifa zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) zimetoa indhari mara chungu nzima kwamba, wananchi wa Yemen wanakabiliwa na maafa makubwa kabisa ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha karne moja iliyopita.
Naibu Wzairi wa Afya wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen anasema, vita, mzingiro na mashambulio ya mabomu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yamepelekea kusambaa naradhi kama malaria, homa ya dengue na kadhalika na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pekee kumeripotiwa matukio 260 ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) imetangaza kuwa, theluthi mbili ya Wayamen ambao ni sawa na watu milioni 20 wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya kibinadamu huku 80% kati yao wakiwa wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Licha ya kuwa dhima ya kile kinachotokea huko Yemen kinapaswa kubebwa na madola vamizi yaani Saudi Arabia na Imarati, lakini kwa mujibu wa uhakiki huru wa kimataifa ni kuwa, Umoja wa Mataifa nao umekuwa mkosa na mhusika na hali hiyo kutokana na kutotekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa. Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na jopokazi huru la kimataifa lililofanya tathmini kuhusiana na hali ya Yemen inaonesha kuwa, licha ya kutengwa dola bilioni 16 na umoja huo katika kipindi cha miaka 7 ya mgogoro wa Yemen, lakini hali ya Yemen ni mbaya mno, na kwa sasa ndio nchi inayokabaliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu ulimwenguni.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano ya Stockholm, Umoja wa Mataifa una jukumu la kuyalazimisha mataifa vamizi kuondoa kikamilifu mzingiro na kufungua njia ya kufikishwa misaada ya kibinadamu. Lakini cha kusitisha ni kwamba, Umoja wa Mataifa umeshindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kama upasavyo na hata kwa namna moja au nyingine unaonekana kuyaandalia mazingira madola vamizi ya Saudia na Imarati kuendelea na malengo yao kwa amani na bila wasiwasi.
Hata hivtyo licha ya kupita miaka saba sasa tangu Saudia ilipoanzisha bila sababu mashambulio ya kijeshi dhidi ya nchi ya Yemen, lakini imeshindwa kufikia malengo yake kutokana na jeshi la Yemen na Kamati za Kujitokea za Wananchi kusimama kidete na kukabiliana na majeshi hayo vamizi. Si hayo tu, bali jeshi la Yemen na kamati za kujitolea za wananchii zimezidi kuimarika siku baada ya siku na hata kuweza kuvurumisha makombora na kutuma ndege zisizo na rubani (droni) ndani ya ardhi ya mataifa hayo vamizi.
Hivi sasa ambapo Saudia na washirika wake zinaonekana kukwama katika kinamasi cha vita huko Yemene na hazina budi isipokuwa kukhitari moja kati ya machaguo haya mawili. Mosi, ima zikubaliane na matakwa ya wananchi wa Yemen ya kuhitimisha vita, kuondoa mzingira na kulipa kufidia ya hasara zilizotokana na vita hivyo. Pili, zisubirie makombora na ndege zisizo na rubani za Wayamen zikitinga katika mataifa yao na kuwatia hasara.