Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameeleza matumaini kuwa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia yatafikia hatua ambayo itakuwa nzuri kwa pande zote mbili na kutengeneza mustakabali mzuri kwa nchi zote mbili.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, IRNA, Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman amesema kwamba Riyadh itaendelea na mazungumzo yake na Iran.
Bin Salman ametabiri mustakbali mzuri wa mazungumzo ya Riyadh mjini Tehran na kusema: “Iran ni nchi jirani na itabaki kuwa jirani yetu milele; hivyo ni vyema kutatua matatizo yaliyopo na kujadili njia za kuishi pamoja.”
Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al-Saud alisema kuwa, Riyadh inasubiri duru ya tano ya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Iran imekuwa ikieleza mara kwa mara utayari wake wa kuendelea na mazungumzo na Saudi Arabia, na kusema kuendelea kwa mazungumzo hayo kunategemea azma ya upande wa pili.
Duru nne za mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia zimefanyika mjini Baghdad nchini Iraq.