Bunge la Ethiopia lapiga kura ya kusitishwa mapema hali ya hatari ya miezi sita

Hatua hiyo ni ishara kwamba mzozo wa umwagaji damu kati ya serikali na vikosi vya waasi wa Tigray unaweza kupungua. Uamuzi wa Bunge la Ethiopia utaanza kutekelezwa hivi karibuni.

Ethiopia ilitangaza hali ya hatari mwezi Novemba mwaka jana baada ya vikosi vya wapiganaji wa Tigray kuvamia maeneo zaidi ya Ethiopia na kutishia mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa.

Hata hivyyo jeshi la serikali mwezi Disemba mwaka jana liliwarudisha nyuma wapiganaji wa Tigray, ingawa mapigano yanaendelea katika eneo la Afar, na Tigray – ambako mamilioni ya raia wanaotegemea msaada – wamesalia bila ya msaada wa chakula tangu katikati ya mwezi Disemba.

Juhudi za kusitisha vita katika taifa hilo la pili kwa ukubwa barani Afrika kwa kiasi kikubwa zimekumbwa na mkwamo, na wanadiplomasia wanaopatanisha kati ya pande hizo mbili wana matumaini finyu ya kupatikana maendeleo baada ya tangazo la kuondolewa hali ya hatari.

Hali hiyo ya hatari nchini Ethiopia iliipa serikali mamlaka ya kuwatia nguvuni raia bila ya kuwafungulia mashtaka na kupekua nyumba bila kibali.

Uamuzi wa Bunge la Ethiopia wa kuondoa hali ya hatari umechukuliwa wiki tatu baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri.

Tesfaye Beljige, msimamizi wa shughuli za serikali bungeni, amewaambia wabunge kwamba hali ya hatari inasababisha uharibifu zaidi kuliko faida zake, akisema sheria hiyyo inakwamisha utalii na shughuli za kiuchumi.

Tathmini iliyofanywa na Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, watu milioni 4.6 ambao ni asilimia 83 kwenye jimbo la Tigray hawana uhakika wa kupata chakula na watu wapatao milioni mbili kati ya hao wamo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na baa la njaa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *