Katika hatua isiyo ya kidiplomasia na inayolenga kushajiisha zaidi fujo na ghasia hapa nchini Iran, Bunge la Umoja wa Ulaya limetangaza kukata uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu.
Katika taarifa, Rais wa Bunge la EU, Roberta Metsola amesema: Katika kujibu vikwazo vya Iran dhidi ya taasisi hii, mawasiliano baina ya jumbe na kamati za Bunge la Ulaya na maafisa wa Iran yamesimamishwa hadi pale maelekezo mengine yatakapotolewa.
Taarifa hiyo imeeleza bayana namna Bunge la Ulaya linapanga kuunga mkono zaidi na kushajiisha ghasia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Bunge la Ulaya amefafanua kwa kusema: Hatutawapuuza na kuwafumbia macho wananchi wa Iran walioko mabarabarani wanaotutazama. Tuko pamoja nanyi, tutabaki kuwa nanyi.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, nchi za Magharibi zimekuwa zikiunga mkono ghasia na machafuko hapa nchini kwa hali na mali, kwa kisingizio cha kifo cha mwanamke wa Kiirani, Mahsa Amini.
Hapo jana Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, kuchochea machafuko na ugaidi nchini Iran si kwa manufaa ya Wamarekani wala nchi za Magharibi na ametoa amri kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuyafuatilia kidiplomasia na kisheria madola yote yaliyohusika na machafuko na vitendo vya kigaidi vya hivi karibuni nchini Iran.