Bunge la Marekani lashindwa kumpata Spika; McCarthy ang’ang’ania licha ya kuangushwa mara tatu

Baraza la Wawakilishi nchini Marekani jana lilishindwa kumpata Spika mpya wa Bunge la nchi hiyo licha ya uchaguzi huo kufanyika mara tatu.

Baada ya duru tatu za upigaji kura, Bunge liliahirisha mchakato huo hadi saa sita mchana leo Jumatano.

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 100 ambapo hakuna Mrepublikan au Mdemokrat aliyeshinda uspika wa Bunge katika duru ya kwanza ya upigaji kura kuwa kiongozi wa baraza lenye wajumbe 435.

Kevin McCarthy kiongozi wa chama cha Republican alishindwa uspika katika awamu tatu za upigaji kura, huku Warepublikan 20 wakimpinga katika duru ya mwisho.

Hata hivyo McCarthy ameapa kusalia katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya hiyo.

McCarthy amewaambia waandishi habari kuwa rais wa zamani Donald Trump alimpigia simu na kusisitiza kumuunga mkono.

Trump anamuunga mkono McCarthy katika kinyang’anyiro hicho na bado ni kiongozi mwenye nguvu katika chama cha Republican.

Wachambuzii wa mambo wanaamini kuwa, mkwamo huenda ukavuruga shughuli za bunge la nchi hiyo kwa kiasi kikubwa na yumkini ukawalazimu wabunge kuangalia mgombea mwingine Mrepublican.

Kiongozi mtarajiwa wa Warepublican bungeni Steve Scalise mwenye umri wa miaka 57 kutoka Louisiana, anaonekana kuwa chaguo jingine. Mara ya mwisho ambayo Bunge la Marekani lilishindwa kumchagua Spika katika duru ya kwanza ilikuwa mwaka 1923.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *