Baraza la mabunge ya nchi wanachama wa shirika la kijeshi la NATO limepitisha azimio ambalo limelitaja shirikisho la Russia kuwa ni ‘dola la kigaidi’.
Kwa mujibu wa tovuti ya chaneli ya CNBC, Yehor Chernov, mkuu wa ujumbe wa kudumu wa Ukraine kwenye baraza la mabunge ya nchi wanachama wa NATO, ametangaza katika taarifa kwamba, katika mkutano wake wa kila mwaka uliofanyika jana mjini Madrid, baraza hilo lilipitisha azimio la kutaka ianzishwe mahakama maalumu kuhusiana na uvamizi wa kijeshi wa Russia dhidi ya Ukraine na kulitangaza shirikisho la Russia kuwa ‘dola la kigaidi’.
Kulingana na taarifa hiyo, nchi 30 wanachama wa NATO zimeunga mkono mapendekezo yaliyowasilishwa na wajumbe wa Ukraine.
Chernov amedai kuwa: kuundwa mahakama hiyo kutawezesha sio tu kushtakiwa wasababishaji wa moja kwa moja wa uhalifu wa kivita, lakini pia viongozi wakuu wa Shirikisho la Russia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, azimio hilo linajumuisha mapendekezo ya kuzidisha utumaji silaha nchini Ukraine na kupanga uchukuaji hatua zaidi za kuiwezesha Ukraine kujiunga na NATO.
Mbali na hatua hiyo, katika mkutano wao huo wa kila mwaka, nchi washirika katika muungano wa kijeshi wa NATO na wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetangaza kuimarisha pia dhamira yao ya kuendelea kutoa misaada ya kudumu na ya muda mrefu ya kijeshi na kifedha kwa Ukraine.
Kabla ya hapo, na katika hatua sawa na ya bunge la NATO, Oktoba 13 Baraza la Bunge la Ulaya nalo pia liliidhinisha kwa kauli moja azimio ambalo lililitaja Shirikisho la Russia kuwa ni ‘dola la kigaidi…/