Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiarabu umelaani hatua ya Uturuki ya kuwakatia maji raia zaidi ya milioni moja wa Syria katika mkoa wa al-Hasakah.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiarabu umetoa taarifa na kutangaza kuwa, kuendelea hatua ya Uturuki ya kukata maji mara kwa mara nchini Syria ni kinyume na misingi ya ujirani mwema na masuala ya kibinadamu, na kulaani utumiaji maji kama silaha dhidi ya raia kwa kisingizio chochote kile.
Umoja wa mabunge ya Waarabu umeonya juu ya madhara hatarishi ya hatua ya Uturuki kwa maisha ya raia wa Syria, na kutaka litafutwe suluhisho la kimsingi na endelevu la kuwadhaminia maji raia wa Syria na kuhitimisha maafa hayo ya kibinadamu yanayowakabili raia hao.
Katika taarifa yao hiyo, wanachama wa Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiarabu wamesisitizia pia uungaji mkono wao kwa juhudi zote za kitaifa, za Kiarabu na kikanda zinazolenga kutafuta suluhisho la mgogoro wa Syria, ambalo litapelekea kupatikana usalama, utulivu na ustawi katika nchi hiyo.