Burkina Faso yamtimua balozi wa Ufaransa nchini humo

Serikali ya Burkina Faso imetangaza kwamba imemtaka balozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou, Luc Hallade, aondoka nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa katika kivumbi cha mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Kufukuzwa kwa balozi Luc Hallade wa Ufaransa kumefanyika wiki mbili baada ya Barbara Manzi, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu nchini Burkina Faso, kutangazwa kuwa mtu asiyefaa na kutimuliwa.

Habari ya kufukuzwa balozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso ilitangazwa jana na msemaji wa serikali, Jean-Emmanuel Ouedraogo.

Hapo awali, serikali ya kijeshi ya Burkina Faso ilikuwa imetangaza katika taarifa yake kuwa imesitisha utangazaji wa Radio France Internationale (RFI) inayofadhiliwa na serikali ya Paris. Sababu ya hatua hiyo ni kueneza taarifa za uongo, na kutangaza habari za upotoshaji.

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso inakituhumu chombo hicho cha habari cha Ufaransa kuwa kinaripoti habari za uwongo na kuyapa jukwaa na sauti magenge ya kigaidi.

Machi mwaka jana pia, nchi nyingine ya Afrika Magharibi, Mali, ilichukua hatua ya kusitisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 kwa tuhuma kuwa vyombo hivyo vya habari vinaripoti habari za uwongo na upotoshaji. Mashirika hayo ya Ufaransa yalidai kwamba jeshi la Mali limeua makumi ya raia.

Kufukuzwa kwa Hallade kunakuja mwaka mmoja baada ya jeshi ya Mali pia kumfukuza balozi wa Ufaransa nchini humo.

Uhusiano wa nchi kadhaa za Magharibi mwa Afrika na Ufaransa umeharibika sana katika miaka ya karibuni.

Burkina Faso ni koloni la zamani la Ufaransa, na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré amekuwa akieleza wazi hisia zake dhidi ya Wafaransa tangu aingie madarakani, na amepanua uhusiano na nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Urusi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *