Burkina Faso yavunja mikataba ya kikoloni ya Ufaransa

Habari kutoka nchini Burkina Faso zinasema kuwa, serikali ya nchi hiyo imevunja mikataba ya kikoloni iliyokuwa imewekwa nchini humo na mkoloni huyo kizee wa Ulaya.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo Jumanne na kumnukuu Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso akisema kuwa, nchi hiyo imevunja mikataba kadhaa na serikali ya Ufaransa ambayo hadi sasa imekuwa ya kinyonyaji na kikoloni kikamilifu. Ni mikataba iliyojali manufaa ya Ufaransa tu bila ya kuwa na faida yoyote kwa wananchi wa Burkina Faso.

Rais Traoré pia amesema: “Kwa kweli kuna mikataba mingi imetiwa saini ambayo inazidi kututumbukiza kwenye lindi la umaskini, serikali yangu imeamua kufuta mikataba hiyo na mashirika ya Ufaransa ikiwa ni hatua ya awali ya kurejesha mali za umma mikononi mwa wananchi wenyewe wa Burkina Faso.”

Amesema, ana yakini kwamba karibuni hivi nchi yake itapata uhuru wake wa kweli inaostahiki kuwa nao na kuongeza kuwa, mapambano hayo hayaihusu Burkina Faso tu, bali ni mapambano kwa ajili ya bara zima la Afrika.

Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso amezidi kuyalaumu madola ya kinyonyaji ya Ulaya Magharibi hasa Ufaransa kwa dhulma na unyonyaji mkubwa zinaozifanyia nchi za Afrika. Lawama zake hizo zimeongezeka hasa baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Niger.

Mara kwa mara Rais Traoré  amekuwa akitoa mwito kwa Waafrika kusimama imara kukabiliana na ukoloni wa madola ya Magharibi.

Hatua hiyo ya serikali ya Ufaransa ya kuvunja mikataba ya kikoloni ya Ufaransa imechukuliwa katika hali ambayo, Jumapili usiku, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa alitangaza kuwa, nchi yake imesimamisha kile alichodai “misaada ya maendeleo” kwa Burkina Faso.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *