Chad yatangaza siku 3 za maombolezo baada ya kuuawa makumi ya wanajeshi

Serikali ya Chad imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya kuuawa makumi ya wanajeshi wake katika jimbo la Lac.

Serikali ya Chad imetangaza kuwa kuanzia leo usiku hadi siku ya Ijumaa bendera zote nchini humo zitapepea nusu mlingoti na hafla na sherehe zote haziruhusiwi kufanyika katika siku za maombolezo.

Vyombo vya habari na maeneo ya ibada yameruhusiwa kutangaza nyimbo na maombi ya kidini tu katika siku tatu za maombolezo.

Watu wasiojulikana waliokuwa na silaha juzi Jumapili waliwashambulia askari usalama katika kambi ya Barkaram katika kisiwa kinachopatikana katika jimbo la ziwa Chad na kuua wanajeshi wasiopungua 40.

Rais Mahamat Idriss Deby wa Chad ameahidi kuwasaka wahalifu hao ambao amesema wamezitumbukiza familia nyingi za Wachadi katika maombolezo.

Chad imekuwa ikipambana dhidi ya wanamgambo wanaobeba silaha katika eneo la ziwa Chad ambapo vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimekuwa vikikabiliana na makundi ya waasi likiwemo kundi la kigaidi la Boko Haram.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *