Chama cha upinzani cha “al Adala wa al Tanmiya” cha Morocco kimelaani ziara ya waziri wa uchumi na viwanda wa utawala wa Kizayuni nchini humo.
Chama hicho kimetoa taarifa rasmi na kusema kuwa kinalaani kwa nguvu zote ziara ya waziri wa uchumi na viwanda wa utawala wa Kizayuni mjini Rabat na pupa ya Morocco ya kuendeleza mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sehemu nyingine ya taarifa ya chama hicho imesema, tunaalaani pia pupa za baadhi ya watu na taasisi za kiutamaduni, kimalezi, kiuchumi na kidini za kujikomba kwa utawala wa Kizayuni na tunatoa onyo kuhusu hatari ya pupa hizo kwa jamii ya Morocco kiutamaduni, kijamii na kisiasa.
Gazeti la Rai al Yaum limeripoti kuwa, chama hicho kiko imara muda wote katika misimamo yake ya kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina kwani kadhia ya Palestina ndilo suala la asili katika umma wote wa Kiarabu na Kiislamu.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, tukiachana na sababu ya kwa nini serikali ya Morocco imetangaza uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Kizayuni, chama cha Uadilifu na Ustawi cha nchi hiyo kimesisitiza kuwa, kitaendelea kuunga mkono muqawama wa Palestina na kitasimama kwa nguvu zake zote kupinga uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Orna Barbivai, waziri wa uchumi na viwanda wa utawala wa Kizayuni yuko nchini Morocco hivi sasa kwa ajili ya ziara rasmi na ziara yake hiyo iliyolalamikiwa vikali inaendelea hadi leo Jumatano.