Changamoto ya nishati na vita vya kuwania madaraka nchini Niger

Licha ya kumalizika muda uliowekwa na ECOWAS kwa baraza la kijeshi la Niger kuhusu kukabidhi madaraka, lakini hakuna ishara zozote zinazoonesha kuwa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya magharibi mwa Afrika iko tayari kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini humo.

Tovuti ya habari ya Al Jazeera imeandika katika ripoti yake kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Niger kwamba: Macho yote yako kwenye hatua itakayochukuliwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo imetishia kutumia nguvu za kijeshi kumkomboa rais aliyepinduliwa na wanajeshi nchini Niger, Mohamed Bazoum, na kumrejesha madarakani.

Kwa mujibu wa Al-Jazeera, muda uliotolewa na ECOWAS kwa wanajeshi wa Niger umemalizika lakini hadi hivi sasa hakuna ishara zozote zinazoonesha jumuiya hiyo itatekeleza vitisho vyake kwa wanajeshi wa Niger.

Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Russia wameonya rasmi dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Oleg Ozerov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia anayehusika na Masuala ya Afrika na mkuu wa Sekretarieti ya Jukwaa la Ubia wa Russia na Afrika, ametangaza kwamba, uingiliaji wowote wa kijeshi wa kigeni katika masuala ya ndani ya Niger utakuwa na matokeo kinyume.

Wakati muhula wa mwisho wa ECOWAS ukimalizika, jana Jumapili makumi ya maelfu ya wafuasi wa wanajeshi waliofanya mapinduzi wakiwa walikusanyika katika uwanja wa michezo wa mji mkuu wa Niger, Niamey, kuwashangilia majenerali wa kijeshi waliofanya mapinduzi hayo ambao wameunda Baraza la Taifa la Kulinda Nchi (CNSP).

Makabiliano kati ya nchi za Magharibi na washirika wao wa kikanda na Russia yameongezeka juu ya mzozo wa kisiasa nchini Niger. Nchi za Ulaya, hususan Ufaransa, ambayo imekuwa na uwepo wa kisiasa na kiuchumi katika nchi hyo ya magharibi mwa Afrika kwa miaka mingi, na taasisi za kikanda kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), zimeitishia Niger kwamba ikiwa wapangaji wa mapinduzi hawatamrejesha madarakani Rais Mohammad Bazoum, wataishambuliai kijeshi nchi hiyo.

Abdel- Fatau Musah, Kamishna wa masuala ya kisiasa na kiusalama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) alinukuliwa kabla ya kumalizika muda wa jumuiya hiyo kwamba: “Mistari ya uingiliaji wa kijeshi tarajiwa dhidi ya utawala wa kijeshi wa Niger, ni moja rasilimali muhimu, pamoja na jinsi na wakati wa kupeleka askari, ni mambo ambayo yamechunguzwa na kuwekwa wazi.

Ufaransa pia imeunga mkono uamuzi huu. Maafisa wa ngazi za juu wa Ufaransa wametangaza kwamba, wanaunga mkono shambulio la kijeshi dhidi ya Niger. Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa alionya kwamba: Wafanya mapinduzi nchini Niger wana hadi leo Jumatatu kumaliza sokomoko lao.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika hali ya sasa, maslahi ya Ufaransa huko Niger na Ukanda wa Sahel Afrika yapo hatarini. Niger ni nchi tajiri na rasilimali zake za urani na dhahabu siku zote zimekuwa zikikodolewa macho ya tamaa na mataifa ya kikoloni. Ni kwa miaka mingi sasa ambapo Ufaransa imekuwa ikitoa sehemu kubwa ya urani inayohitajika kwa mitambo yake kutoka nchi hii, lakini sasa maslahi ya Ufaransa na washirika wake yamekuwa hatarini.

Onyo la shambulio la kijeshi la Ufaransa na washirika wake dhidi ya Niger na linakuja wakati nchi kama Mali na Burkina Faso zimetangaza rasmi kwamba zinachukulia shambulio lolote dhidi ya Niger kama vita dhidi yao. Vitisho hivi vimesababisha waliopanga mapinduzi ya Niger kuomba msaada kutoka kwa kundi la Wagner ili kudumisha mamlaka yao.

Uhalisia wa mambo ni kuwa, filihali Niger imekuwa uwanja wa ushindani kati ya nchi za Ulaya na Russia. Russia ambayo imekuwepo katika nchi mbalimbali za Afrika kwa muda mrefu, imepanua uwepo wake katika nchi mbalimbali za bara hili katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya vita vya Ukraine.

Nchi nyingi za Kiafrika, kama vile Algeria na Libya, ni wauzaji wa nishati, hasa ya gesi kwa nchi za Ulaya. Kwa msingi huo, Russia inajaribu kudhibiti soko la nishati ya Ulaya kwa kuwepo katika nchi hizi na kuongeza mashinikizo kwa nchi hizi katika kudhamini nishati.

Katika fremu hiyo, Niger pia ni moja ya nchi zinazosambaza urani kwa Ulaya, haswa Ufaransa, kwa hivyo, baada ya vikwazo vya Ulaya dhidi ya Russia nafasi ya Niger katika suala la usambazaji wa nishati kwa Ulaya imeongezeka na kuwa mahali pa ushindani na kupimana misuli bila kificho baina ya madola makubwa ulimwenguni.

Hivi sasa mapinduzi hayo yamesimamisha upelekaji wa madini ya urani kwa Ufaransa, na kwa kuimarishwa hisia dhidi ya Ufaransa huko Niger, kumeongezeka matakwa ya nchi za eneo hilo ya kumaliza ukoloni wa Ufaransa. Hata kama suala hilo linahesabiwa kuwa mshtuko mkubwa kwa Ufaransa na Ulaya, lakini inaonekana kuwa, hali hii imetoa fursa kwa Russia kufanya mabadiliko ya kimataifa katika sera za nishati na kuwa na mahudhurio hai na amilifu zaidi barani Afrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *