Katika mkutano na viongozi wa bara la Afrika, Rais Xi Jinping wa China aliahidi kutoa msaada wa kifedha wa dola bilioni 50 kwa bara hili katika miaka mitatu ijayo.
Akihutubia mkutano mkubwa zaidi wa kilele wa Beijing tangu janga la coronavirus, Xi aliahidi kutoa zaidi ya dola bilioni 50 kwa Afrika katika miaka mitatu ijayo na kuahidi kuimarisha ushirikiano katika miundombinu na biashara na bara hilo, kulingana na shirika la habari la Xinhua
Zaidi ya wakuu 50 wa nchi za Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wamehudhuria mkutano wa wiki hii kati ya China na Afrika.
Viongozi wa Afrika wiki hii walitia saini mikataba mingi ya ushirikiano zaidi katika miundombinu, kilimo, madini, biashara na nishati.
Katika sherehe za ufunguzi wa Kongamano la China na Afrika kwenye Ukumbi Mkuu wa Watu wa Beijing Alhamisi asubuhi, Xi Jinping alisifu uhusiano na bara la Afrika kuwa “kipindi bora zaidi katika historia”.
Amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta ya viwanda, kilimo, miundombinu, biashara na uwekezaji.
Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, serikali ya China iko tayari kutoa msaada wa kifedha wa Yuan bilioni 360 (dola bilioni 50.7) kwa Afrika, alisisitiza Xi.
Rais wa China alisema kuwa zaidi ya nusu ya misaada hii itakuwa katika mfumo wa mkopo wa kiasi cha dola bilioni 11 “katika aina mbalimbali za misaada”, pamoja na dola bilioni 10 kupitia kuhimiza makampuni ya China kuwekeza.
Pia aliahidi kusaidia kuunda angalau nafasi za kazi milioni moja barani Afrika.
Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amewaambia wakuu wa nchi za Afrika katika mkutano huu kwamba uhusiano unaokua kati ya China na bara hili unaweza kuendeleza mapinduzi ya nishati mbadala.
China ikiwa nchi nambari mbili kwa uchumi duniani, ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa bara la Afrika na imejaribu kutumia rasilimali asilia za bara hilo zikiwemo shaba, dhahabu, lithiamu na madini adimu.
Beijing imetoa mabilioni ya mikopo kwa nchi za Afrika na kusaidia kujenga miundombinu inayohitajika.
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, alitangaza baada ya mikutano hiyo Jumatano kwamba makubaliano yalifikiwa kati ya kampuni ya umeme ya serikali ZESCO na Beijing PowerChina kupanua matumizi ya paneli za jua za paa nchini mwake.
Nigeria na China zilitia saini taarifa ya pamoja ambapo walikubaliana “kuongeza ushirikiano” katika miundombinu, ikiwa ni pamoja na usafiri, bandari na maeneo ya biashara huria.
Kwa upande wake, Rais wa Tanzania Samia Sulehu Hassan aliahidi kusukuma mbele maendeleo mapya katika njia ya reli inayounganisha nchi yake na nchi jirani ya Zambia.
Mradi huu, ambao vyombo vya habari vya Zambia vilisema Beijing imeahidi dola bilioni 1, unalenga kupanua viungo vya usafiri katika sehemu ya mashariki ya bara la Afrika.