Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema utawala wa Israel lazima ukomeshe “uchochezi na chokochoko” dhidi ya Wapalestina, hususan katika mji wa al-Quds (Jerusalem) huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Qin Gang amesema, “Tunautaka upande wa Israel kuacha uchochezi na kujizuia kuchukua hatua yoyote ya upande mmoja ambayo inaweza kupelekea hali kuwa mbaya zaidi.”
Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Misri mjini Cairo.
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Israel imeongeza mashambulizi katika miji ya Palestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Kutokana na mashambulizi hayo makumi ya Wapalestina wamepoteza maisha na wengine wengi kukamatwa.
Umoja wa Mataifa umeutaja mwaka 2022 kama mwaka mbaya zaidi kwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi katika kipindi cha miaka 16.
Wanajeshi katili wa Israel waliwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 171 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds Mashariki inayokaliwa kwa mabavu mwaka jana, wakiwemo zaidi ya watoto 30. Takriban wengine 9,000 walijeruhiwa pia.
Qin Gang amesisitiza kuwa, “Rais Xi Jinping wa China hivi karibuni alisisitiza kwamba ukandamizaji wa kihistoria wanaofanyiwa watu wa Palestina haupaswi kuendelea kwa muda usiojulikana na kwamba haki halali na za kitaifa za Wapalestina hazipaswi kuathiriwa.”
Pia aliitaka jumuiya ya kimataifa kusukuma “mazungumzo ya amani” kati ya Wapalestina na Waisraeli na kutafuta “suluhisho la haki na la dharura kwa kadhia ya Palestina.”
Wapalestina wanasema wanataka Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa sehemu ya taifa huru la baadaye la Palestina, na mji mkuu wake ukiwa ni ni al-Quds Mashariki. Duru ya mwisho ya mazungumzo kati ya Israel na Palestina ilisambaratika mwaka 2014. Miongoni mwa mambo makuu yaliyopelekea mazungumzo kusambaratika hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuendeleza ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni.