Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China ameitaka serikali ya Marekani ibadilike na iache kukandamiza maendeleo ya China.
Wang Yi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China amesema kuwa, Marekani haipaswi kuendeleza utaratibu wake wa zamani wa uonevu wa upande mmoja.
Wang ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na kueleza bayana kwamba, Washington inapaswa kubadilika.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China amebainisha kuwa, Marekani lazima izingatie masuala halali ya China. Wang amesisitiza kwamba nchi hizo mbili zinapaswa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, G20 mjini Bali, Indonesia baina ya Rais wa China, Xi Jinping, na mwenzake wa Marekani, Joe Biden.
Wang amesema ni muhimu kuongeza mashauriano juu ya mwongozo wa kanuni za uhusiano kati ya China na Marekani, kuimarisha mazungumzo katika nyanja zote na kutatua masuala muhimu kati ya nchi hizi mbili.
Mvutano kati ya China na Marekani umechukua mkondo na wigo mpana zaidi katika miaka ya hivi karibuni ambapo mataifa hayo mawili yamekuwa yakituhumiana katika masuala mbalimbali.
Hivi karibuni, Marekani ilipeleka meli zake mbili za kivita kwenye Lango Bahari la Taiwan. Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China, na imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan; na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.