Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imelalamikia vikali safari ya Bettina Stark-Wattsinger, Waziri wa Elimu wa Ujerumani katika Kisiwa cha Taiwan na kusisitiza kuwa inapinga safari rasmi ya waziri huyo katika kisiwa hicho kinachomilikiwa na serikali ya Beijing.
Wakati huo huo, ubalozi wa China mjini London umelaani safari ya wabunge kadhaa wa Uingereza katika kisiwa cha Taiwan na kuitaja kuwa ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya China, jambo ambalo linatuma ujumbe usio sahihi kwa watu wanaotaka kujitenga katika kisiwa hicho.
Katika miaka ya hivi karibuni na hasa baada ya urais wa Donald Trump nchini Marekani na kufuatia ziara ya Nancy Pelosi, spika wa zamani wa Congress ya nchi hiyo katika kisiwa cha Taiwan mapema Agosti 2022, hali ya wasiwasi imeongezeka katika eneo hilo. Sambamba na kuongezeka mashinikizo ya kisiasa na kijeshi ya Marekani dhidi ya China, ziara za maafisa wa nchi za Magharibi katika kisiwa cha Taiwan zimeongezeka sana. Kwa hakika, suala la Taiwan na kuungwa mkono harakati za kujitenga kisiwa hicho limekuwa moja ya mashinikizo yanayotumiwa na nchi za Magharibi, hasa Marekani, dhidi ya serikali ya Beijing.
Safari ya hivi karibuni ya viongozi na wawakilishi wa Ujerumani na Uingereza huko Taiwan ni jaribio la nchi za Magharibi kuonyesha kuwa zimeunda umoja dhidi ya China. Beijing inakichukulia kisiwa cha Taiwan kuwa sehemu muhimu ya ardhi yake na hivyo inapinga vikali hatua yoyote ya kukitenganisha na ardhi-mama ya China.
Li Ming, mtaalamu wa masuala ya kijeshi katika kisiwa hicho, anasema kuhusu mipango ya nchi za Magharibi kwa kisiwa hicho na jibu la China kwamba: “Nchi za Magharibi kwa kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiusalama kuhusiana na Taiwan, zinatarajia China kutoa majibu mawili; la kwanza ni kuzingira na kuishinikiza kijeshi Taiwan na la pili ni kwa nchi hiyo kuanzisha mashambulio ya kijeshi ya pande zote dhidi ya kisiwa hicho. Kwa mtazamo wa nchi hizo, iwapo China itaamua kufuata njia ya kwanza, itakabiliwa na matokeo yale yale ya kimataifa sawa na ya kukishambulia moja kwa moja, na hilo ndilo lengo la Marekani.”
Wakati huohuo, Li Haidong, profesa katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Mahusiano ya Kigeni cha China, pia anaamini kwamba: “Warepublican na Wademokrat wa Marekani wote wanajaribu kutumia suala la Taiwan kama chombo cha kuidhibiti China, ambapo sasa serikali ya Washington ina mipango ya kutuma misaada zaidi ya kijeshi kwa Taiwan, jambo ambalo linaweza kuwa na matokeo yasiyotabirika.”
Kile kinachojadiliwa hivi sasa katika duru za kisiasa na kifikra katika nchi za Magharibi na hasa nchini Marekani ni kutekelezwa huko Taiwan mfano wa vita vinavyoendelea nchini Ukraine ili kuitumbukiza China katika mtego wa vita vya Taiwan. Kuhusu suala hilo, wachambuzi wa kijeshi na masuala ya kigeni katika Kituo cha “Usalama wa Marekani Mpya” au kwa kifupi CNAS, wamechunguza hali na majibu tofauti ambayo yanaweza kutolewa na China kuhusu Taiwan, kupitia adharia bandia waliyoipa jina la “chura mwenye sumu” ambapo iwapo China itashambulia na hatimaye kuiunganisha Taiwan na ardhi yake mama, italazimika kwanza kukishambulia kisiwa kidogo cha Taiwan kinachoitwa Dongsha kilichoko katika Bahari ya Kusini ya China. Kisiwa hicho ambacho kwa sasa kiko katika udhibiti wa Taiwan, kina nafasi muhimu katika kudhamini maslahi ya China katika eneo hilo.
Suala hilo linathibitisha wazi kwamba nchi za Magharibi, hasa Marekani, zinatekeleza njama tofauti kuhusu Taiwan ili kuitumbukiza China katika mtego wa kukishambulia kisiwa hicho na hivyo kuifanya itumie sehemu kubwa ya nguvu na uwezo wake katika kukitetea kisiwa hicho, ikiwa ni katika jitihada zake za kulinda mamlaka na umoja wa ardhi yake. Katika uwanja huo Henry Kissinger, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa ambaye pia ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani ameitahadharisha mara kwa mara serikali ya Washington kuhusu hatari ya kushinikizwa kupita kiasi, Beijing, hususan kuhusiana na suala zima la kisiwa cha Taiwan.