China yaondoa vizuizi vyote vya Covid-19 kwa wasafiri

Serikali ya China imetangaza kufungua tena mipaka yake kwa wageni wa kimataifa kwa mara ya kwanza tangu ilipoweka vizuizi vya kusafiri mnamo Machi 2020 kufuatia janga la corona.

Wasafiri wanaoingia hawatahitaji tena kuwekewa karantini hatua ambayo inaashiria mabadiliko makubwa katika sera ya serikali ya Beijing ya Covid-19. Tangazo hilo linatolewa katika hali ambayo, kwa sasa China inapambana na ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 hali ambayo imezua wasiwasi.

Hata hivyo wasafiri wanaoingia China bado watahitaji uthibitisho wa kipimo hasi cha (PCR) kilichofanyika ndani ya saa 48 za kusafiri. Hatua hiyo imekaribishwa na wengi wanaotamani kuungana tena na familia zao.

Jumapili ya jana mabasi ya ghorofa yaliyojaa wasafiri yalifika katika Daraja la Hong Kong-Zhuhai-Macau ili kuelekea mkoa wa Guangdong – miongoni mwao walikuwa wanafunzi wa chuo waliokuwa wakirejea nyumbani.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, kuna matumaini kwamba janga la dunia nzima la ugonjwa wa Covid-19 litamalizika katika mwaka huu wa 2023.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni katika jedwali la dunia nzima la Corona, Marekani ndiyo inayoongoza kimaafa kwa kuwa na watu milioni 102,963,370 walioambukizwa virusi vya corona na 1,120,040 walioaga dunia kwa ugonjwa huo, ikifuatiwa na India yenye watu milioni 44,680,402 walioambukizwa.

Janga la ulimwengu mzima la corona liliikumba dunia tangu mwanzoni mwa 2020. Ripoti za kwanza kuhusu mripuko wa ugonjwa huo zilitangazwa mjini Wuhan nchini China mnamo Desemba 2019.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *