China yathibitisha kumtia mbaroni jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA

Serikali ya China imethibitisha kupitia taarifa kwamba imemgundua na kumkamata jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).

Awali vyombo vya habari vya China vilitangaza kugunduliwa raia wa China anayetuhumiwa kuifanyia ujasusi CIA. Saa kadhaa baadaye duru rasmi za nchi hiyo zilithibitisha habari hiyo.

Wizara ya Usalama ya China imetangaza katika taarifa kwamba raia huyo Mchina aliyetajwa kwa jina la Zeng alikuwa mfanyakazi wa kitengo cha jeshi la nchi hiyo kinachohusika na masuala ya ufundi na aliajiriwa na wakala mmoja wa CIA nchini Italia kulifanyia ujasusi shirika hilo.

Zeng alipelekwa Italia na kitengo hicho cha jeshi la China kwa ajili ya utafiti ambako alikutana na kujuana na ajenti huyo wa CIA.

Taarifa ya wizara ya usalama ya China imeendelea kueleza kuwa, baada ya ajenti huyo wa CIA “kumteteresha” Zeng kwa upande wa itikadi za kisiasa alianza kukusanya taarifa nyeti kuhusu jeshi la China kupitia jasusi huyo.

Jasusi huyo mpya wa CIA alipewa mafunzo ya ujasusi kabla ya kurejea China.

Imeelezwa kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani lilikuwa limemuahidi Zeng kitita kikubwa cha pesa na fursa ya uhamiaji yeye na familia yake kuelekea Marekani mkabala wa taarifa za ujasusi alizotakiwa kulipatia shirika hilo.

Mnamo mwezi Julai mwaka huu, China ilipanua wigo wa sheria zake za kupambana na ujasusi huku Marekani ikionyesha kutiwa wasiwasi na hatua hizo zilizochukuliwa na Beijing.

Aidha, mapema mwezi huu serikali ya China iliwaomba raia wake washiriki katika shughuli za kukabiliana na ujasusi ili kuunga mkono usalama wa taifa. Beijing imepanga kutoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kuwahamasisha raia wake kutoa ushirikiano juu ya suala hilo…

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *