Televisheni ya CNN imetangaza katika ripoti yake kwamba Ukraine imegeuzwa kwa “maana halisi” maabara ya kufanyia majaribio silaha za Marekani.
Televisheni hiyo ya Marekani imeeleza katika ripoti yake kuwa, hakuna silaha yoyote ya Magharibi ambayo “kabla ya hapo imetumika katika mapigano kati ya mataifa mawili yaliyoendelea kiviwanda,” kwa maana hiyo Ukraine imegeuzwa kuwa “maabara ya majaribio ya silaha kwa maana kamili ya neno hilo.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vita vya Ukraine vimekuwa chanzo kikubwa cha taarifa kuhusiana na mifumo ya Marekani.
CNN imemnukuu afisa mmoja wa Pentagon ambaye hakutajwa jina na kueleza kwamba kwa miaka mingi ijayo viongozi wa kijeshi watatalii data na taarifa kuhusiana na Ukraine.
Ripoti hiyo ya CNN imeendelea kueleza kwamba, Jim Himes, mbunge wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani ameeleza kuhusiana na suala hilo kwamba: “kitabu kizima kinaweza kuandikwa kuhusu mafunzo tuliyopata kutokana na vita vya Ukraine”.
Tangu vilipoanza vita nchini Ukraine Februari 24, 2022, nchi za Magharibi zimetuma msaada mkubwa wa fedha, silaha na zana za kijeshi kwa nchi hiyo.
Kwa upande wa Marekani, imeipatia serikali ya Kyiv msaada wa zaidi ya dola bilioni moja na kuwa moja ya waungaji mkono wakubwa zaidi wa serikali hiyo katika vita baina yake na Russia.
Russia imeshatoa wito mara kadhaa wa kuzitaka nchi za Magharibi zikomeshe kile ilichokiita “umiminaji” wa silaha kwa Ukraine, na kutahadharisha kuwa kuendelea kwa mwenendo huo kutarefusha zaidi muda wa mgogoro kati ya Moscow na Kyiv na kusababisha mateso zaidi kwa raia nchini Ukraine.