Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeiomba jamii ya kimataifa kuiwekea vikwazo nchi jirani ya Rwanda ikiituhumu kuwasaidia waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Patrick Muyaya, amesema kuwa kamwe hatajadiliana na kundi la M23, ingawa kundi hilo limesisitiza kuwa liko tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Muyaya amesema: “Tunachokiomba kwa jamii ya kimataifa ni rahisi. Wanaweza kutumia vikwazo kuiweka Rwanda mashinikizo ili iacha inachokifanya mashariki mwa DRC.”
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema: “Tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha usalama wa watu wa Goma na Sake, mashariki mwa nchi.”
Mapema mwezi huu, Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilifanikiwa kuzima jaribio la kundi la waasi wa M23 la kutaka kudhibiti mji wa Sake ulioko kilomita 27 kutoka Goma, mashariki mwa taifa hilo.
Mwezi uliopita pia Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23.