Kiwanda kipya cha kusafishia mafuta cha Dangote nchini Nigeria ni kikubwa zaidi barani Afrika – na kitazalisha mapipa 650,000 ya petroli kwa siku, na kukipa uwezo wa kushughulikia tatizo la usambazaji wa nishati katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na mfanyabiashara wa viwanda wa Nigeria na mtu tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, kilizinduliwa Jumatatu na kinatarajiwa kuongeza uwezo wa usafishaji mafuta ndani ya nchi hiyo, ili kuondokana na upungufu uliopo. Pia kinatazamiwa kupunguza utegemezi wa nje na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kiwanda kipya cha kusafishia mafuta cha Dangote ni cha kwanza cha kusafisha mafuta ghafi kinachomilikiwa na mtu kibinafsi nchini Nigeria. Viwanda vya kusafishia mafuta vilivyopo Nigeria, vilivyokumbwa na matatizo makubwa ya utendaji kazi vinamilikiwa na serikali na vimeshindwa kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya bidhaa za petroli. Pamoja na kuwa Nigeria ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta ghafi ya petroli kwa wingi duniani, lakini nchi hiyo imekuwa ikiagiza mafuta ya petroli yaliyosafishwa kutoka nchi za Ulaya.
Kwa sasa Nigeria inaagiza zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zake za petroli iliyosafishwa. Nchi hiyo ndiyo muagizaji mkubwa zaidi wa bidhaa za petroli iliyosafishwa barani Afrika. Kwa hivyo uzalishaji wa ndani utapunguza sana muswada wa uagizaji wa bidhaa nchini.
Mnamo 2021, Nigeria ilitumia dola bilioni 11.3 kuagiza bidhaa za petroli iliyosafishwa. Nigeria inatoa ruzuku kwa bei ya pampu ya petroli. Kwa kuwa nchi inaagiza kutoka nje sehemu kubwa ya bidhaa zake za petroli iliyosafishwa, inalazimika kutoa ruzuku ya petroli ili kupunguza athari za kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Rais Muhammadu Buhari alisema kuanzishwa na kuzinduliwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangoti katika eneo la Ibeju-Lekki katika jimbo la Lagos, kitovu cha uchumi cha Nigeria, ni dalili ya kuwa mataifa yanaweza kupata mafanikio makubwa iwapo wafanyabiashara wanasaidiwa.