Chama cha The Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini kimesema hakiombolezi kifo cha Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza aliyefariki jana.
Taarifa ya EFF imesema Elizabeth alichukua hatamu za uongozi Uingereza mwaka 1952, na kutawala kwa miaka 70 kama mkuu wa ufalme ambao ulidumishwa na urithi wa kikatili wa kudhalilisha utu wa mamilioni ya watu duniani kote.
Taarifa hiyo imesema: “Hatuombolezi kifo cha Elizabeth, kwa sababu kwetu kifo chake ni ukumbusho wa kipindi cha kutisha sana Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.”
Taarifa hiyo imekumbusha kuhusu jinai za utawala wa kikoloni wa Uingereza nchini Afrika Kusini ambapo utajiri ulioporwa nchini humo ulitajirisha familia ya kifalme ya Uingereza.
EFF imeongeza kuwa ni familia ya kifalme ya Uingereza iliyoidhinisha vitendo vya Cecil John Rhodes, kupora utajiri Zimbabwe na Zambia. Aidha chama hicho cha mrengo wa kushoto Afrika Kusini kimesema ilikuwa ni familia ya kifalme ya Uingereza iliyofaidika na mateso na ukatili dhidi wa watu wa Kenya waliokuwa wakipambana kishujaa dhidi ya ukoloni wa kijinai wa Uingereza.
Taarifa hiyo imesema: “Nchini Kenya, Uingereza ilijenga kambi za mateso na kukandamiza kwa ukatili wa kinyama mwamko wa Mau Mau, na kumuua Dedan Kimathi tarehe 18 Februari 1957, wakati Elizabeth alikuwa tayari Malkia.”
Chama hicho za upinzani Afrika Kusini kimesema familia ya kifalme Uingereza pia ilipora India kupitia Kampuni ya East India na ilichukua udhibiti na kuwakandamiza watu wa visiwa vingi vya eneo la Caribbean. EFF imesema kiu ya utajiri ya Ufalme wa Uingereza ilisababisha njaa na kupelekea mamilioni ya watu kufa huko Bengal, na ubaguzi wao wa rangi ulisababisha mauaji ya kimbari ya watu wa asili huko Australia.
Chama cha EFF kimesema wakati wa utawala wake wa miaka 70 kama Malkia, hakuwahi kukiri hata mara moja ukatili ambao familia yake iliwafanyia watu kote ulimwenguni. Taarifa hiyo imesema Malkia Elizabeth wa Pili alinufaika kutokana na utajiri uliopatikana kutokana na ukandamizaji na mauaji ya mamilioni ya watu duniani kote.