Erdogan: Borrell hana mamlaka ya kuzungumzia uhusiano wa Uturuki na Russia

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema: Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya hana mamlaka ya kuzungumzia uhusiano wa Uturuki na nchi zingine ikiwemo Russia.

Erdogan amesema matamshi aliyotoa hivi karibuni Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kuhusu uhusiano wa Ankara na Moscow ni za kuchukiza na akasisitiza kwamba: “Borrell hana mamlaka ya kuhukumu na kutoa maoni kuhusu sera za nje za Uturuki.
Rais wa Uturuki ameongezea kwa kusema: “Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya hana mamlaka ya kutupangia uhusiano wetu wa Russia”.
Erdoğan ametoa matamshi hayo baada ya Joseph Borrell kuliandikia barua Bunge la Ulaya akisema, anatia wasiwasi na kuendelea kwa ushirikiano kati ya Russia na Uturuki.
Katika barua yake hiyo, Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya ameilaumu Uturuki kwa kutotoa ushirikiano katika utekelezaji wa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na akabainisha kwamba, Ankara inajaribu kuchukua nafasi ya muunganishi wa kibiashara kwa bidhaa za Russia zilizosusiwa ili kuisaidia nchi hiyo kukwepa vikwazo ilivyowekewa na Brussels.

Serikali ya Uturuki imekataa kujiunga na mpango wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na kujaribu kuchukua nafasi ya mpatanishi kati ya nchi hiyo na Ukraine.

Wakati huo huo, Rais wa Uturuki ametangaza leo kuwa Russia imekaribisha pendekezo la nchi hiyo la kufanyika mkutano wa pande tatu za Uturuki, Russia na Syria na akaeleza kwamba anataka uandaliwe utaratibu wa pamoja kati ya Ankara, Damascus na Moscow kwa ajili ya kupambana na ugaidi katika eneo.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *