Ethiopia imekosoa kufanyika kwa kikao maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kujadili na kutathmini visa vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo kufuatia mzozo unaoendelea kati ya serikali na waasi wa Tigray.
Faraan: Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa Zenebe Kebede amelishutumu baraza hilo akisema limetekwa na fikra za kikoloni na linatumika kisiasa.
Kebede ameongeza kuwa nchi hiyo inaandamwa na inatuhumiwa na Baraza la Haki za Binadamu kutokana na kutetea serikali yake iliyochaguliwa kidemokrasia na kulinda amani na mustakabali wa watu wake.
Hii ni kufuatia hatua ya nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la UN kutaka kutumwa wachunguzi wa kimataifa nchini Ethiopia ili kuchunguza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu kaskazini mwa nchi hiyo katika mgogoro ambao unaendelea kwa mwezi wa 13 sasa.
Mapigano kati ya serikali kuu ya Ethiopia na Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF ya eneo hilo la kaskazini mwa nchi yameibua mzozo wa kisiasa nchini humo. Vita na mapigano ya ndani katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia vinavyoendelea kwa muda wa karibu mwaka mmoja sasa vimepelekea maelfu ya watu kuuawa, zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi na kuwafanya wengine zaidi ya laki nne kukabiliwa na baa la njaa.
Mgogoro, kung’ang’ania madaraka, uchaguzi na msukumo wa mageuzi ya kisiasa ni miongoni mwa mambo yametajwa kuwa yanachangia machafuko nchini Ethiopia…/