Ethiopia imeziangusha Tanzania na Uganda na kuwa nchi inayoongoza kwa uwekezaji wa Wakenya wanaowekeza nje ya nchi.
Takwimu mpya zinaonyesha kuwa uwekezaji wa moja kwa moja wa Kenya nchini Ethiopia ulifikia Ksh60.2 bilioni (dola milioni 440.7) mwaka wa 2021—na hivyo kuzipita Tanzania ambayo ilipokea uwekezaji wa Dola milioni 377 na Uganda dola milioni 412.
Utafiti mpya wa Kiuchumi wa 2023 uliotolewa unaonyesha kuwa ingawa Tanzania ilikuwa nchi inayoongoza katika kuwavutia wawekezaji wa Kenya wanaowekeza nje ya nchi hadi kufikia mawaka 2015, sasa Wawekezaji wanaelekea Ethiopia.
Kampuni kadhaa za Kenya ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya mawasiliano ya Safaricom zimejitosa katika soko la Ethiopia ambapo inafanya kazi chini ya kampuni tanzu ya Safaricom Telecommunications Ethiopia Private Limited (STE).
Uzinduzi wa hatua kwa hatua wa Safaricom Ethiopia ulianza mnamo Agosti 2022 katika jiji la Dire Dawa na utaenea hadi miji mingine 24, pamoja na Addis Ababa katika miezi inayokuja.
Benki za Kenya, ikiwemo Benki ya KCB, zimeonyesha nia ya kutaka kuingia katika soko la Ethiopia. Ujumbe wa watendaji wakuu kutoka Benki ya KCB ulitembelea Tume ya Uwekezaji ya Ethiopia (EIC) mjini Addis Ababa Oktoba mwaka jana ambapo ulifanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Ethiopia.