Faili la sauti lililovuja la mwandishi wa BBC: Lengo la machafuko ni kuigawa Iran

Faili la sauti lililovuja la mwandishi wa shirika la utangazaji la Uingereza BBC limefichua wazi jinsi Magharibi na vyombo vyao vya habari zinavyotekeleza njama ya kuigawa Iran.

Maandamano yaliyoibuka hivi karibuni nchini Iran kwa kisingizio cha kifo cha “Mahsa Amini” kwa mara nyingine tena yamewafanya maadui wa kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia tukio hilo kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kuzusha machafuko kadiri wawezavyo.

Katika ghasia za hivi karibuni, viongozi wa kisiasa wa Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya na vyombo vyao vya habari, vimetumia vibaya tukio hilo kuyaunga mkono magenge yanayozusha ghasia na kuvuruga usalama kwa kaulimbiu ya kuunga mkono haki za watu wa Irani na eti kutetea haki za wanawake.

Hata hivyo katika faili lililovuja la sauti la matamshi ya mwandishi wa BBC Persian, Rana Rahimpour, mwandishi huyo anasikika waziwazi akisema kuwa lengo la ghasia na machafuko ya nchini Iran ni kusambaratisha Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, lengo nyuma ya pazia la wafanya ghasia sio demokrasia, bali ni kuigawa Iran katika vipande kadhaa.

Katika faili hilo la sauti, Rahimpour anaeleza wazi kwamba televisheni ya lugha ya Kifarsi ya Saudi Arabia iliyopachikwa jina la Iran International imetakiwa kuwapa ukumbi na jukwaa viongozi wa makundi na vyama vyenye fikra ya kugawanywa ardhi ya Iran.

Rana Rahimpour mwenyewe amethibitisha usahihi wa faili hilo la sauti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Faili hilo lililovuja ni miongoni mwa uthibitisho wa wazi zaidi kutoka kwa waandishi wa vyombo vya habari vya nchi zinazoipinga Iran kuhusu chanzo cha ghasia za hivi karibuni nchini na hujuma na propaganda ya vyombo vya habari kama vile BBC, CNN na Iran International.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *