Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amelitaja shambulio la ndege za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza kuwa ni kilele cha uungaji mkono wa Washington kwa jinai na uhalifu unaofanywa na utawala huo.
Ni baada ya ndege za kivita za Israel kushambulia kambi ya wanamapambano wa Wapalestina huko Gaza mapema leo Jumamosi, masaa machache tu baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kutembelea utawala huo haramu.
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesisitiza kuwa: Mashambulizi ya leo ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza ambayo yamefanyika moja kwa moja baada ya ziara ya Rais Joe Biden wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ni kielelezo cha kilele cha uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo unaohamasisha uhalifu zaidi dhidi ya watu wa Palestina.
Msemaji wa Hamas amewasifu mujahidina wa harakati hiyo ya mapambano waliokabiliana na ndege za kivita za Israel na kuzilazimisha kuondoka kwenye anga ya Gaza na akasema kuwa muqawama wa kishujaa wa Palestina utalilinda taifa hilo.