Fedheha ya ubaguzi wa rangi katika mchezo wa soka barani Ulaya

Ubaguzi wa rangi ni silaha ya tangu na tangu, ambayo siku hizi, na licha ya kauli mbiu zote za kuwepo usawa baina ya watu wote na haki za binadamu kwa wote, ingali inatumiwa katika Ulimwengu wa Magharibi dhidi ya watu weusi na wasio Wazungu. Siku hizi katika nchi za Magharibi, watu wa rangi zingine hasa weusi, hawana hadhi sawa na weupe, licha ya wanavyojituma na michango mingi mno wanayotoa.

Pamoja ya kuwepo mifano mingi na ya wazi ya ubaguzi huo wa rangi, hivi karibuni, ulimwengu wa michezo barani Ulaya umeonyesha moja ya taswira chafu na chungu zaidi ya ubaguzi wa rangi mbele ya macho ya walimwengu.

Wakati wa mechi ya soka iliyochezwa Jumapili usiku tarehe 13 Mei kati ya Real Madrid na Valencia, mashabiki wa Uhispania wa timu ya Valencia walimwandama nyota Mbrazil wa timu ya Real Madrid Vinicius Junior kwa matusi ya ubaguzi wa rangi, kiasi kwamba matusi hayo yalimfanya Vinicius ashindwe kuficha huzuni na majonzi yaliyompata akabubujikwa na machozi wakati mechi hiyo ikiwa inaendelea.

Kuanzia dakika za awali kabisa za mechi hiyo, maelfu ya mashabiki waliokuwepo kwenye Uwanja wa Mestalla walimtukana Vinicius kwa kauli chafu za udhalilishaji, huku wachezaji wa timu ya Valencia wakiungana nao pia kufanya hivyo uwanjani humo mpaka wakafanikiwa kumchochea mchezaji huyo atolewe nje ya uwanja kwa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili cha mchezo. Kutolewa uwanjani Vinicius Junior kulikoambatana na hasira na huzuni za mchezaji huyo nyota wa soka, kwa mara nyingine tena kumedhihirisha kwa uwazi kabisa ubaguzi wa rangi uliovunda katika jamii za Magharibi.

Mkasa huo wa kusikitisha umezigusa na kuzitonesha hisia za walimwengu katika nchi nyingi duniani ambao wameonyesha waziwazi jinsi kitendo hicho kilivyowachukiza na kuwaumiza. Sambamba na hayo, baadhi ya viongozi na maafisa wa nchi mbalimbali wameuelezea muamala wa ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinicius Junior kuwa ni “uhalifu wa chuki” na kutaka zichukuliwe hatua kali kuukomesha.

Rais Lula da Silva wa Brazil, amemuunga mkono raia wake na kusema: “Sio haki kwa masikini kijana huyu, ambaye sasa hivi ni mmoja wa wachezaji bora wa soka duniani, aandamwe na matusi katika kila uwanja wa michezo aendako.” Rais wa Brazil ameendelea kusema: “hatuwezi kuruhusu ufashisti na ubaguzi wa rangi uchukue udhibiti wa viwanja vya soka”.

Silvio Almeida, Waziri wa Haki za Kibinadamu wa Brazil, yeye pia amesema: “tabia ya viongozi wa Uhispania na taasisi zinazosimamia soka ya nchi hiyo ni za kihalifu. Hii inaonyesha kuwa wameukubali ubaguzi wa rangi”.

Kufuatia kuzuka kwa tukio hilo, wanasoka wengi mashuhuri duniani wakiwemo Benzema, Mbappe, Ederson na Neymar pamoja na vilabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Flamengo ya Brazil wamemuunga mkono Vinicius mwenye umri wa miaka 22 dhidi ya matusi ya ubaguzi wa rangi ya mashabiki wa Valencia.

Beki wa zamani wa Uingereza Rio Ferdinand amehoji kwa uchungu, “ni mara ngapi zaidi Vinícius akabiliwe na mambo kama haya. Ninaona uchungu, ninaona karaha, ninahisi anahitaji msaada … na viongozi hawafanyi lolote”.

Japokuwa miamala ya dharau na ya kibaguzi dhidi ya watu weusi ni ya muda mrefu sana barani Ulaya, lakini jamii za Magharibi hasa za Ulaya zimekuwa zikiipigia upatu na kuitetea kauli mbiu ya usawa kati ya wanadamu wote na utoaji fursa sawa kwa watu wote. Viongozi wa Ulaya wamekuwa wakizungumzia kila mara kuheshimiwa haki za binadamu na hata kwenda mbali zaidi kwa kusikika mara nyingi wakizishutumu na kuzituhumu nchi zingine hasa mataifa manyonge yanayoendelea kwamba yanakiuka haki za binadamu na kutoa kauli za kuyakaripia na hata kuyaadhibu.

Hii ni pamoja na kuwa katika nyuga za kijamii, kisiasa na hata michezo, watu wasio Wazungu katika nchi za Magharibi hawana usalama wa maisha na wa kupata haki sawa na raia wengine. Maudhi na unyanyasaji wanaofanyiwa wahalifu weusi na Polisi katika nchi za Ulaya na matusi na udhalilishaji wanaofanyiwa watu weusi makazini ni miongoni mwa masaibu hayo. Kuhusiana na hilo, Almaz Tafra, mtafiti wa haki za binadamu, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa mtafiti maalumu wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, ameandika katika ripoti yake: “watu wa Ulaya wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi katika maisha yao ya kila siku”.

Mechi ya soka kati ya Real Madrid na Valencia imeonyesha kwa mara nyingine tena kuwa ubaguzi wa rangi lingali ni suala muhimu barani Ulaya.

Baada ya yaliyojiri Jumapili usiku katika uwanja wa Mastalla, kocha mkuu wa Real Madrid, Carlo Ancelotti aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “leo ilikuwa siku ya huzuni huko Mastalla, mahali ambapo kundi moja la mashabiki lilionyesha sura yao mbaya zaidi. Ni wakati wa kuacha kusema tu na kuchukua hatua madhubuti. Ubaguzi wa rangi hauna nafasi katika soka na katika jamii. ‘Hapana’ kwa ubaguzi wa rangi mahali popote pale”.

Alaa kulli hali na pamoja na yote hayo, hakuna ajuaye kama tabia na miamala ya ubaguzi wa rangi iliyoonyeshwa dhidi ya mchezaji huyo wa timu ya soka ya Real Madrid haitarudiwa tena katika siku za usoni dhidi ya wanamichezo wengine wasio Wazungu barani Ulaya…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *