FIFA yakataa ombi la Rais wa Ukraine la kutangazwa ujumbe wake kabla ya mechi ya fainali

Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) inadaiwa limekataa ombi la Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kutaka kabla ya kuchezwa mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na Ufaransa siku ya Jumapili irushwe hewani video yake uwanjani hapo ili kuhamasisha amani.

Inadaiwa kuwa Zelensky aliomba hilo huku akitaka kuonekana katika video hiyo akitoa ujumbe wa kuhamasisha amani wakati huu nchi yake ikiwa katika vita na jirani yake Russia.

Taarifa za ndani kutoka baadhi ya vyombo vya habari za michezo zinaeleza kuwa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) limemkatalia Zelensky ombi lake hilo pasipo kumpa sababu.

Rais wa Ukraine amekuwa akihutubia kwa njia mbalimbali katika matukio makubwa duniani kuhusu amani ikiwa inatafsiriwa kama ishara ya kuomba uungaji mkono katika vita dhidi ya Russia.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema shirikisho hilo la soka duniani limechukua hatua ya kusimamisha baadhi ya “taarifa za kisiasa” nchini Qatar kwa sababu linapaswa “kumzingatia kila mtu.”

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Doha hapo jana, Infantino alisisitiza kwa kusema: “Sisi ni shirika la ulimwengu mzima na hatubagui mtu yeyote”.

Rais huyo wa shirikisho la kandanda ulimwenguni amebainisha: “tunatetea maadili, tunatetea haki za binadamu na haki za kila mtu kwenye Kombe la Dunia. Hao mashabiki na mabilioni wanaotazama kwenye televisheni, wana matatizo yao. Wanachotaka tu ni kutazama dakika 90 au 120 bila kufikiria juu ya chochote, bali kufurahia tu muda huo mdogo wa raha na furaha. Inabidi tuwape muda ambapo wataweza kusahau matatizo yao na kufurahia soka.”

Kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Dunia, rais huyo wa FIFA alitoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Ukraine kwa muda wote wa mashindano hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *