Filippo Grandi atembelea kivuko cha mpaka kati ya Misri na Sudan, kukagua juhudi za kutoa misaada

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi jana Jumapili alitembelea kivuko cha mpaka wa Misri na Sudan na kuangalia juhudi za misaada zinazotolewa na UNHCR na Misri.

Hayo yameripotiwa na televisheni ya taifa ya Misri ambayo pia imesema: Filippo Grandi aliishukuru serikali ya Misri kwa kupokea maelfu ya Wasudan na watu wengine wanaokimbia “machafuko mabaya” nchini Sudan.

Jumuiya ya Madaktari wa Sudan ilisema jana Jumapili kwamba, mapigano ya silaha yamekuwa yakiendelea kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi tangu Aprili 15, na kusababisha hadi sasa raia 866 kuuawa na wengine 3,721 kujeruhiwa.

Akiwa kwenye kivuko hicho, Grandi alisema: “Wajibu wangu wa kwanza kabisa hapa ni kutoa mwito kwa wanajeshi wanaopigana Sudan. Acheni kupigana. Ikiwa kweli mnajali watu wenu, basi tafadhalini acheni kupigana, kwa sababu watu wenu ndio wanaoteseka.

Grandi aliandamana na gavana wa jimbo la kusini mwa Misri la Aswan wakati wa ziara yake kwenye kivuko hicho cha mpakani.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi alisema siku ya Jumamosi kuwa nchi yake imepokea hadi sasa raia 150,000 wa Sudan wanaokimbia mzozo unaoendelea nchini kwao.

Rais huyo wa Misri ametoa mwito kwa mashirika ya misaada na mataifa wafadhili kutoa msaada unaohitajika kwa nchi jirani za Sudan ili kuziwezesha kuendelea na jukumu lao la kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi wa Sudan.

Mkuu huyo wa UNHCR aliwasili Misri siku ya Jumamosi kwa ziara ya siku tatu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *