Rais Ali Bongo wa Gabon amemteua Waziri Mkuu wa nchi hiyo Rose Christiane Ossouka Raponda kushika wadhifa wa makamu wa rais ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanamke kushika wadhifa huo kama ambavyo ameteua pia Waziri Mkuu mpya kuchukua nafasi ya Raponda.
Uteuzi huo ulioripotiwa jana, ulifanyika siku ya Jumatano ambapo Waziri Mkuu wa Gabon Rose Christiane Ossouka Raponda, 59, ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu mwezi Julai 2020 baada ya mtangulizi wake kujiuzulu, sasa “atamsaidia” mkuu wa nchi. Taarifa iliyotolewa kuhusu uteuzi huo imesisitiza kuwa, Raponda ni Makamu wa Rirais wa kwanza mwanamke nchini humo.
Waziri mwingine wa zamani, Alain-Claude Bilie-By-Nze, atachukua nafasi ya Ossouka Raponda na Uwaziri Mkuu na jukukmu la kuunda serikali mpya. Hayo yamesema na Kkatibu Mkuu wa Rais Bongo Jean-Yves Teale alisema katika taarifa yake kwa njia ya video na ambayo imewekwa kwenye ukurasa wa Twitter ya Rais Ali Bongo.
Bilie-By-Nze, 55, ni mshirika wa karibu wa Rais Bongo a ameshikilia nyadhifa kadhaa za uwaziri tangu 2006. Siku hiyo hiyo ya Jumatatu, alitangaza serikali yake yenye mawaziri 45 bila mabadiliko yoyote katika nyadhifa muhimu.
Wakati akiwa Waziri Mkuu, Bi Ossouka Raponda alilazimika kuvuka mazingira magumu ya kisiasa baada ya jaribio la mapinduzi la mwaka wa 2019 wakati Rais Ali Bongo alipokuwa kwenye likizo ya muda mrefu ya matibabu ya ugonjwa wa kiharusi.
Gabon ni nchi ambayo imetawaliwa na familia moja kwa zaidi ya miongo mitano sasa. Kiutaalamu Bi Raponda ni mtaalamu wa uchumi kutoka Taasisi ya Uchumi na Fedha ya Gabon na amebobea katika masuala ya fedha za umma.