Gazeti la Uhispania: Mechi ya Iran na Marekani ni mpambano mkubwa wa kisiasa

Gazeti la Marca la Uhispania limeitaja mechi ya soka ya michuano ya Kombe la Dunia kati ya timu ya taifa ya kandanda ya Iran na Marekani kuwa ni mpambano mkubwa wa kisiasa.

Timu ya taifa ya kandanda ya Iran itamenyana na timu ya taifa ya Marekani katika mechi ya tatu ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kesho Jumanne usiku katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Al-Thamamah. Katika mechi zake mbili za mwanzo, timu ya Iran ilijipatia pointi tatu na timu ya Marekani ilipata pointi mbili. Mshindi wa mechi hiyo atafuzu kuingia kwenye hatua ya mtoano ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia ya 2022 inayofanyika nchini Qatar.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, gazeti la Marca linalochapishwa nchini Uhispania limeandika makala maalumu kuhusu pambano kati ya timu ya taifa ya Iran na Marekani likisema: mechi hii si shindano la michezo tu bali ni mpambano mkubwa wa kisiasa, ambao ulianzia hapo awali katika Kombe la Dunia la 1998 nchini Ufaransa. Katika mechi hiyo Iran ilifanikiwa kumshinda mpinzani wake kwa mabao mawili kwa moja.

Ripoti ya gazeti la Marca imegusia pia miongo minne ya uhusiano mbaya wa kisiasa ambao umekuwepo kati ya Iran na Marekani.

Gazeti hilo la Uhispania limeendelea kueleza kuwa: vita vya kisaikolojia vilianza tangu jana na hata Marekani ikaondoa nembo ya “Allah” iliyopo katikati ya bendera ya Iran na kukabiliwa na upinzani wa nchi hiyo.
Kufuatia hatua hiyo ya kiuadui ya Marekani, tovuti rasmi ya Shirikisho la Soka la Iran, ilituma baruapepe kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA kulitaka litoe angalizo na kulichukulia hatua kali Shirikisho la Soka la Marekani.
Mvutano kati ya timu hizo mbili na rabsharabsha zinazohusiana na mechi hiyo ya kesho vimeshuhudiwa waziwazi hata katika mikutano ya waandishi wa habari.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *