Serikali ya Somalia ilitangaza jana Jumamosi kwamba genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab limeomba kufanya mazungumzo na serikali hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa genge hilo kuomba kukutana na kuzungumzo na serikali ya Mogadishu.
Ombi hilo la al Shabab limekuja huku vikosi vya serikali vikiendelea kupambana na genge hilo kigaidi ambalo limetangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaidah.
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Somalia Abdifatah Qasim ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, genge la kigaidi la al Shabab halina nafasi ya kufanya mazungumzo na serikali, isipokuwa raia wa Somalia ambao ni wanachama wa genge hilo wanaweza kuruhusiwa kufanya mazungumzo hayo.
Waziri Qasim amesema: “Kuna makundi mawili ndani ya al Shabab. Sehemu ya kwanza ni wageni, na sehemu ya pili ni Wasomali wenyeji ambao wako kwenye genge hilo. Wale wenyeji wana nafasi ya kufanya mazungumzo nasi, lakini wale wageni waliovamia nchi yetu hawana haki ya mazungumzo. Chaguo pekee ni kurejea walikotoka.”
Matamshi yake yametolewa mbele ya waandishi wa habari katika mji mkuu wa Mogadishu, siku moja baada ya genge la kigaidi kufanya mashambulizi makali dhidi ya vikosi vya serikali katika kijiji cha Hilowle Gaab kusini mwa mkoa wa Shabelle ya Kati.
Shambulio hilo ni la pili kwa ukubwa kufanywa na genge hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2023.
Siku ya Jumatano, genge hilo la ukufurishaji lilishambulia mji wa Mahas katika mkoa wa Hiran, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 35.
Al Shabab imekuwa ikifanya mashambulio dhidi ya serikali ya Somalia na vikosi vya kimataifa tangu angalau 2007 na kusababisha maafa makubwa.