Gesi inavyobana matumizi na kufungua fursa

Mtwara. Matumizi ya gesi asilia kwenye malori 256 ya kiwanda cha saruji cha Dangote yamesaidia kuokoa takriban Sh5 bilioni iwapo magari hayo yangetumia mafuta kati ya Machi 2021 hadi Juni.

Uchambuzi uliozingatia mwenendo wa bei za mafuta katika siku za hivi karibuni, kiwanda hicho kingetumia zaidi ya Sh11 bilioni lakini gesi imeokoa asilimia 45 ya kiasi hicho.

Mbali na magari, kiwanda hicho pia kinatumiza gesi asilia kuendesha mitambo yake ya uzalishaji saruji ikitengeneza kilowati 750 za umeme kutokana na asilimia 10 ya gesi inachonunua kutoka kituo cha kusindika gesi hiyo kilichopo Madimba mkoani Mtwara.

Madimba ndio kituo kikubwa kinachozalisha futi milioni 210 za ujazo kwa siku kupitia visima vitano, vinne vikiwa Mnazibay na kimoja huko Msimbati chini ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC).

Hata hivyo, wakati kiwanda hicho kikinufaika, Serikali inayosimamia miradi hiyo imekiri kuwa bado haijaanza kutumia gesi hiyo kwenye magari yake 15,742 na pikipiki 14,047 pamoja na mitambo 373 huku Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiagiza magari ya Serikali kuzimwa yanapoegeshwa ili kubana matumizi kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Meneja wa kituo cha kusindika gesi kiwandani hapo, Francis Simon alisema matumizi ya gesi asilia yanaokoa asilimia 45 ya gharama za mafuta hatua iliyowashawishi kuagiza malori mengine 150 yaliyofungwa mfumo huo.

Hatua hiyo ina akisi kanuni za bei ya gesi asilia za mwaka 2016, zinaoonyesha matumizi ya gesi hiyo katika magari, viwandani na nyumbani huokoa takribani asilimia 40 ya mapato ambayo yangetumika katika n mafuta. Hii ni sawa na kupunguza Sh40 katika kila Sh100 inayotumika.

“Manufaa ni makubwa sana, tuna mpango wa kuleta magari mengine 150 mwaka huu na kujenga kituo cha kujaza gesi jijini Dar es Salaam ili gari linapotoka huku likiishiwa gesi lijaze huko (Mtwara) wakati wa kurudi kiwandani,” alisema Simon.

Simon alibainisha hayo wiki iliyopita alipozungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara kiwandani hapo kuangalia usambazaji w anishati hiyo chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura).

Lori moja la kiwanda hicho hujazwa mita za ujazo 185 za gesi asilia ambazo ni sawa na lita 166.5 za mafuta na kuweza kusafiri wastani wa kilometa 700.

Kauli ya TPDC

Alipoulizwa endapo wanaishauri Serikali kuona umuhimu wa kutumia gesi katika magari yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Dk James Mataragio alisema wanajenga vituo vya kujaza gesi kwenye magari (CNG).

Aggrey Jimmy, meneja mauzo wa kanda ya Dar es Salaam alisema gesi imepunguza gharama za uzalishaji lakini changamoto za kupanda kwa bei ya dizeli imekwamisha mipango ya kutekeleza ahadi ya kushusha bei ya saruji hiyo hadi Sh8,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Alisema kiwanda hicho kinachangia kati ya asilimia 27 hadi 30 ya saruji yote inayozalishwa nchini huku ikiwa na ushindani mkubwa wa bei katika masoko ya kanda ya kaskazini, kusini, na Dar es Salaam.

“Gesi imepunguza karibu nusu ya bei lakini bado tuna asilimia karibu 70 ya magari tunakoyoyadi kwa ajili ya shughuli za kiwandani ambayo hutumia mafuta. Kwa hiyo gharama za uzalishaji bado zinaathiriwa na mafuta lakini gesi ni tumaini la kushusha bei,” alisema Jimmy.

Hali ya uzalishaji

Matumizi ya gesi asilia katika kiwanda cha Dangote ni sehemu ya uzalishaji wa futi za ujazo milioni 210 kwa siku kutoka visima vya Madimba inayotegemea visima vinne vya Mnazibay na kimoja cha Msimbati.

Hussein Chitemo, menaja uzalishaji wa kampuni ya utafiti na uendelezaji wa gesi asilia ya Maurel&Prom Limited alisema tayari futi za ujazo bilioni 125 kati ya trilioni 1.4 kimechimbwa katika visima vitano vya Kitalu cha Mnazibay tangu mwaka 2006.

“Tuna wateja wawili kwa sasa tunapozalisha futi milioni 93 za ujazo kwa ajili ya kampuni ya Gasco inayosambaza majumbani na futi milioni 3.3 za ujazo kwa ajili ya Tanesco Mtwara wanaozalisha megawati 16 za umeme,” alisema Chitemo.

Charles Nyangu ambaye ni mkuu wa kitengo cha ushirikishaji wazawa na uhusishaji wa wadau kutoka Pura alisema leseni ya kampuni hiyo itakoma mwaka 2031 lakini mkataba unatoa nafasi ya kampuni hiyo kuongezewa muda wa kuendeleza shughuli zake kutokana akiba ya kiasi cha gesi kilichopo.

Mwitikio kitaifa

Siku chache zilizopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchismi Mramba alinukuliwa katika mdahalo wa mtandaoni kuhusu matumizi ya gesi akisema zaidi ya Watanzani 300 kwa mwezi wanabadili mfumo wa magari yao ili yatumie gesi kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia.

Licha ya viwanda zaidi ya 40 vilivyounganishwa pamoja na maelfu ya magari kupitia bomba la gesi jijini Dar es Salaam, asilimia 60 ya umeme unaozalishwa na kutumika nchini unazalishwa kutokana na rasilimali hiyo.

Vilevile, kuna zaidi ya makazi 2,000 mkoani Lindi, Mtwara na Dar es Salaam yaliyounganishwa kutumia nishati ambayo hazina iliyopo inaonyesha Tanzania ina akiba ya fiti trilioni 57.5 za ujazo zinazotosha kuinua uchumi wa nchi.

Taarifa za TPDC zinaonyesha kilo 0.65 za gesi iliyosindikwa ambayo ni sawa na lita 1.54 ya petroli inatosha kulipeleka gari umbali wa kilomita 12. Wakati beiya lita moja ya petroli ikiwa takriban Sh3,000 ile ya kilo moja ya gesi asilia ni Sh1,550 tu.

Isihaka Mchinjita, msemaji wa kisekta wa sekta ya nishati wa Chama cha ACT Wazalendo alisema Serikali inatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwashawishi Watanzania na viwanda kutumia gesi kwenye magari.

“Matumizi ya gesi yanatunza injini na matengenezo huwa kidogo sana, Serikali inataka kupunguza matumizi kwa Sh500 bilioni kati ya Sh558 bilioni iliyokuwa inatumia, hiyo inayobaki inaweza kupungua zaidi endapo magari ya Serikali yatatumia gesi. Hiyo ndio tafsiri ya unafuu wa gesi,” alisema.

Ripoti ya mpango wa matumizi ya gesi asilia Tanzania wa mwaka 2016 hadi 2045, inaonyesha futi trillioni 8.8 za ujazo zinatarajiwa kutumika kuzalisha umeme wakati futi trilioni 0.5 zikitumika kwenye kaya, futi trilioni 3.6 zikitumika kwenye viwanda na futi trilioni 0.6 kwenye magari katika kipindi hicho.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *