Alphabet, ambalo ni shirika mama la kampuni ya intaneti ya Kimarekani ya Google limetangaza kuwa litawafuta kazi wafanyakazi zaidi ya 12,000.
Sundar Pichai, Afisa Mkuu Mtendaji wa Alphabet amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kampuni hiyo imeshuhudia mawimbi mazito ya kimapato kutokana na mdororo wa uchumi, na kwa msingi huo wanalazimika kuwafuta kazi wafanyakazi 12,000.
Alphabet ilikuwa na takriban wafanyakazi rasmi 187,000 kote duniani kufikia Disemba 2022, na kufutwa kazi watu 12,000 kutamaanisha kukoseshwa ajira asilimia 6 ya wafanyakazi hao.
Kupungua ukuaji wa uchumi na kuongezeka mfumuko wa bei huko Marekani pamoja na kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo yameilazimisha kuamua kuachisha kazi idadi kubwa ya wafanyakazi wake.
Haya yameripotiwa siku moja baada ya shirika la Microsoft kusema kuwa litapunguza wafanyakazi 10,000 katika miezi ijayo. Aidha mapema mwezi huu wa Januari, Mkurugenzi Mtendaji wa Amazon alisema kuwa kampuni hiyo itawafuta kazi wafanyakazi zaidi ya 18,000.
Baadhi ya waajiri wakubwa wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Walmart, Facebook, Twitter na Pepsi, hivi karibuni wamepunguza maelfu ya nafasi za kazi nchini humo kutokana na kuzorota kwa uchumi.