Guterres: Afrika ni sehemu muhimu ya biashara na uwekezaji duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Afrika ni sehemu muhimu ya biashara duniani na eneo kubwa la uwekezaji.

Guterres ameyasema hayo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa uzinduzi wa mpango wa kimataifa wa kuimarisha biashara barani Afrika, Global African Business Initiative, GABI,  wenye lengo la kuchagiza fursa za kibiashara na kukwamua bara hilo kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Afrika ya sasa haishikiki na haizuiliki kwa kuwa ina mambo mengi ya kuchangia, “kila sekta ya uchumi AFrika inakua, kuanzia uzalishaji, kilimo, huduma hadi fedha.”

Amesema vijana katika bara hilo ni nguvu kazi chipukizi na soko kubwa la watumizi na biashara na kwamba “Eneo la biashara huru barani Afrika litachochea uwekezaji na fursa za biashara.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema mwelekeo chanya wa Afrika unakwamishwa na majanga na changamoto ambazo bara hilo halijasababisha.

 “Kuanzia COVID-19 na majanga ya tabianchi, hadi vita ya Ukraine. Kuanzia kongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa, janga la ongezeko la gharama za maisha na kurudi nyuma kwa maendeleo katika kufanikisha na kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGc,” amesema Katibu Mkuu bila kusahau mfumo wa fedha duniani ambao amesema umeundwa kwa makusudi ili kuikwamisha Afrika na hivyo lazima mfumo huo ufanyiwe marekebisho ya kimsingi.

Guterres amesema lakini sasa wamekutana pamoja kwa sababu wanafahamu wakati umefika wa kuchukua hatua kwa kuzingatia simulizi mpya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Afrika ni  eneo lililosheheni fursa nyingi na rasilimali, huku wanawake, vijana na waafrika walio ughaibuni nao wakijumuishwa katika harakati za kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi barani humo.

Katibu Mkuu amesema kwa kuongozwa na Ajenda 2030 ya maendeleo endelevu na Ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika, mabadiliko hayo  ya chanya yatafikiwa.

Ametaja maamuzi ya kijasiri ambayo yataweka SDGs katika kitovu ya miundo ya kibiashara, akitolea mfano mathalani wa mafuta ya kisukuku.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *