Guterres: Dunia inaitegemea Afrika kutatua shida zake lakini haiisaidii Afrika kukabili changamoto zake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema suala la kusikitisha ni kuwa, licha ya kwamba dunia inaitegemea Afrika kutatua shida zake, lakini bado bara la Afrika halijaweza kuweka tegemeo lake kwa dunia katika kukabili changamoto zinazolikabili.

Guterres amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari, ambao umehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, AU Moussa Faki Mahamat.

Katibu Mkuu wa UN ambaye yuko jijini Addis Ababa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa AU ametolea mfano madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba Afrika, kuanzia ukame hadi mafuriko, vichocheo vikiwa ni shughuli za uchafuzi zinazosababishwa na mataifa makubwa.

“Afrika inapokea matone tu ya usaidizi kukabili na kuhimili uharibifu huu,” amesema Katibu Mkuu na kubainisha kuwa, mamia ya watu wamepoteza maisha na mamilioni wamepoteza makazi yao kutokana na mafuriko ya hivi karibuni Nigeria, Chad na Sudan Kusini  na akaongezea kwa kusema: “na hili ni kumbusho juu ya kushindwa kwetu kushughulikia janga la tabianchi.”

Kwa mantiki hiyo Guterres amependekeza mambo makuu matatu ya kurejesha imani ya Afrika kwa dunia na wakati huo kusukuma mbele maendeleo na kukabili athari za tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwepo ubia mpya kwa ajili ya ustawi na maendeleo na kufafanua kuwa, nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika zinahitaji msaada wa dharura kuimarisha huduma na miradi inayohitaji.

Guterres amekumbusha pia kuwa Afrika inahitaji na ina haki ya usaidizi kwenye tabianchi na kueleza kwamba, hatua ya COP27 kuanzisha Mfuko Maalumu wa kufidia hasara na uharibifu ni hatua muhimu katika kufikia haki kwenye tabianchi hasa kwa wale ambao wanaathirika bila kusababisha, Afrika ikiwa mojawapo.

Jambo la tatu aliloashiria Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni haki na hitajio la amani ililonalo bara la Afrika. Amelifafanua hilo kwa kusema, kuanzia Sahel hadi Maziwa Makuu na hadi Ethiopia, mizozo bado ni changamoto, na kwamba wamezungumza kwenye mkutano Addis Ababa ni kwa vipi Umoja wa Mataifa na AU wanaweza kushirikiana kuimarisha amani Afrika sambamba na haki za binadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *