Pele, mchezaji mashuhuri wa soka wa Brazil ambaye anatajwa kuwa mwanasoka bora zaidi katika historia, ameaga dunia.
Edson Arantes do Nascimento almaarufu Pele, alfariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, familia yake imetangaza Alhamisi.
Hospitali ya Albert Einstein iliyoko mjini Sao Paulo, ambako Pele alikuwa akipokea matibabu, imesema gwiji huyo wa kandanda alifariki saa tisa na dakika 27 alasiri kwa saa za Brazil, kutokana na viungo vyake kushindwa kufanya kazi. Pele amekuwa akiugua saratani ya utumbo.
Kifo cha Pele, ambaye ni mtu pekee aliyeshinda Kombe la Dunia la FIFA mara tatu kama mchezaji mwaka 1958, 1962 na mwaka 1970, kilithibitishwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram.
Bintiye Pele, Kely Nascimento ameandika katika Instagram kwamba: “Kitu kizuri kutoka kwetu ni kukupongeza. Tunakupenda sana. Pumzika kwa amani.”
Pele alizaliwa mjini Tres Coracoes nchini Brazil mnamo Oktoba 23, 1940.
Pele aliondoka kwenye umaskini hadi kuwa mmoja wa wanasoka wakubwa na wanaojulikana sana katika historia. Aliibeba Brazil hadi kwenye kilele cha soka na kuwa balozi wa kimataifa wa mchezo huo katika safari iliyoanzia mitaa ya jimbo la Sao Paulo, ambapo alicheza mpira wa kutengenezwa na soksi iliyojaa magazeti au matambara.
Pele a anabakia kuwa kinara wa ufungaji wa timu ya taifa akiwa amefunga mabao 77 katika mechi 92. Nyota wa sasa wa Brazil, Neymar, alifikisha magoli hayo kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu nchini Qatar, akifunga bao lake la 77 katika michezo 124.
Serikali ya Rais Jair Bolsonaro, anayeondoka madarakani mnamo siku ya Jumapili, imetangaza siku tatu za maombolezo, na kusema katika taarifa kuwa Pele alikuwa mzalendo halisi, akiliinua jina la Brazil kila mahali alipokwenda.
Mrithi wa Bolsonaro, Rais mteule Luiz Inacio Lula da Silva, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa, “Wabrazil wachache sana wamefanikiwa kulibeba jina la nchi yetu kama alivyofanya Pele.”
Vigogo mbali mbali wa soka duniani wametuma salamu zao za rambirambi. mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG) Kylian Mbappe amemuomboleza Pele akisema atakumbukwa milele. “Mfalme wa kandanda hayuko nasi tena lakini mafanikio yake hayatasahaulika. Pumzika kwa amani,” ameandika Mbappe kwenye ukurasa wa akaunti yake ya Twitter.
Naye Fowadi matata wa Ureno Cristiano Ronaldo kupitia Instagram ametuma salama za pole si tu nchini Brazil na hasa kwa familia ya Pele, lakini pia kwa dunia nzima.